Search This Blog

Friday, August 12, 2011

MSIMU MUHIMU KWA WACHEZAJI HAWA

Wakati mashabiki wa soka wakijiandaa kuukaribisha msimu mpya wa soka kwenye ligi kuu nchini England ni vyema tukawatazama baadhi ya wachezaji ambao wana madeni ya kulipa kwa mashabiki wa timu wanazochezea.




Aaron Ramsey (Arsenal)




Arsenal wamekumbwa na balaa la majeruhi ya wachezaji wake katika nyakati tofauti, majeraha haya yamewatia baadhi ya wachezaji vilema vya maisha kiasi kwamba japo wanacheza lakini hawachezi katika kiwango kile kile walichokuwa wanacheza kabla ya kuumia ,


Aaron Ramsey februari mwaka 2010 alivunjika mifupa miwili ya tibia na fibula kwenye mguu wake baada ya kugongana na Ryan Shawcross. Ramsey alivunjika vibaya kiasi kwamba hata Ryan Shawcros mwenyewe ambaye alipewa kadi nyekundu japo ni dhahiri hakukusudia alitoka uwanjani huku machozi yakimtiririka.


Mungu si Athumani Ramsey alirejea uwanjani mwezi Novemba mwaka huo huo akiwa kwenye klabu ya Nottingham Forest kwa mkopo. Ramsay aliporudi uwanjani mwanzoni alionekana kuwa tofauti na hakuwa Ramsey Yule wa siku zote. Japo uwezo wake wa asili ulikuwepo, alikuwa anaonekana dhahiri kuathirika kisaikolojia kutokana na jeraha alilopata miezi tisa nyuma.


Ila wazungu wana msemo usemao “time is a healer” yaani muda ni tiba tosha na ndio kilichotokea kwa Aron kwani aliutumia vyema muda wake akiwa na Nottingham Forest na alirejea Arsenal mwezi machi , Ramsey alionyesha kile walichokikosa mashabiki wa Arsenal muda aliokosekana kwa bao safi alilofunga kwenye mchezo dhidi ya Manchester United mwezi mei na bao lingine kwenye kombe la Emirates limewapa wana Arsenal matumaini zaidi .


Jeraha la Aaron lilikuwa kama la Eduardo lakini bahati nzuri kwa Aaron ni kuwa ameweza kurejea kwenye kiwango chake kile kile na wakati huu ambao huenda Arsenal ikawapoteza viungo wake wawili muhimu Samir Nasri na Cesc Fabregas inaweza kuwa nafasi muhimu kwa Ramsey kuingia na kuchukua mojawapo ya nafasi hizi mbili na kuwapa Arsenal malipo ya imani yao kwake .





Stephen Ireland (Aston Villa)

Japo kuna wiki kadhaa zimebakia kabla hajasherehekea kutimiza umri wa miaka 25 , Stephen Ireland anaonekana kama mtu aliyecheza ligi kuu ya England kwa muda mrefu sana kiasi cha kuwa mkongwe , hii ni kwa sababu katika kipindi kifupi ameweza kupanda na kushuka baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa 2008/09 wa Manchester City.


Kitu ambacho kimemtatiza sana Ireland ni imani ndogo waliyo nayo makocha kwake. Mwezi Novemba mwaka 2008 alimtaja kocha Mark Hughes kama mmoja wa makocha bora aliowahi kucheza chini yao, lakini kufikia Februari mwaka 2010 Hughes huyo huyo alikuwa akilaumiwa kwa kushuka kiwango cha Ireland sababu kuu ikitajwa ni kumchezesha Ireland katika nafasi ambayo si yake .


Ireland alimtaja Roberto Mancini kuwa ndiye aliyemrejesha kwenye kiwango chake, lakini mwezi Agosti mwaka 2010 huyo huyo Ireland akamponda Mancini kwa kushindwa kujenga mahusiano mazuri na wachezaji wake.
Stephen Ireland aliondoka Man City na kujiunga na Aston Villa na ndani ya muda mfupi kocha aliyemnunua Martin O’neal aliondoka na aliyekuja kuchukua nafasi yake Gerard Houllier hakuwa na mpango naye .


Houllier alisema kuwa Ireland anahitaji kufanyia kazi soka lake ; Ireland alijibu mapigo kwa kusema kuwa katika mara chache alizocheza alicheza vizuri na mfano ni mechi ya Chelsea ambako alikuwa “Man of the match” ila Houllier hakuliona hilo.


Mwisho wa siku Stephen Ireland alipelekwa Newcastle United kwa mkopo “ Ireland alizungumzia uhamisho wake kwa mkopo kwa maneno haya ‘kwa mara ya kwanza niko chini ya kocha ambaye anihitaji kwenye timu yake’ lakini cha ajabu ni kuwa mpaka kufikia mwisho wa mkataba wake wa mkopo Alan Pardew aliamua kuwa hamhitaji Ireland Newcastle ambako alicheza mechi mbili tu huku muda mrefu akiwa majeruhi.
Kocha mpya wa Aston Villa Alex McLeish ameonekana kuwa tayari kumpa nafasi Ireland. McLeish amesema kuwa Ireland amekuwa na bahati mbaya sana kwa kuwa mambo hayajamuendea vyema ila uwezo aliounyesha kwenye mazoezi umempa imani kuwa anastahili kupewa nafasi na ana imani kuwa atarejesha fomu aliyokuwa nayo. Ni wakati wa Ireland kuwadhihirishia makocha wake wa siku za nyuma kuwa walikuwa na makosa kwa kutomuamini.




Fernando Torres (Chelsea)

Mshindi wa kombe la dunia akiwa na timu yake ya taifa ya Hispania na mchezaji ghali kuliko wote nchini England , sifa zote hizi Fernando Torres hakuzitendea haki na katika miezi yake sita akiwa na Chelsea iliyomnunua toka Liverpool alifunga bao moja tu.


Torres alikuwa na wakati mgumu sana mwaka 2010, pamoja na kwamba alivaa medali ya ushindi kwenye timu ya taifa lakini ukweli ni kwamba Torres alikuwa abiria tu kwenye ndege ya Hispania akiwasindikiza wenzake kwani hata kwenye fainali aliingia kama mchezaji wa akiba na baadaye alitolewa akiwa ameumia .


Dalili za Torres wa zamani kurejea zilionekana akiwa na Liverpool lakini lilipokuja dirisha dogo aliuzwa kwenda Chelsea ambako bundi alionekana kumuandama tena . Torres alionekana kama mpotevu kwenye kikosi cha Chelsea .


Jukumu la kucheza pamoja na Didier Drogba lilionekna gumu kwake huku kila mmoja kati yake na Drogba akifanya kila awezalo kuudhihirishia uongozi kuwa usajili wake haukuwa sahihi (kwa drogba) na kwa upande wake ulikuwa sahihi. Kwa ufupi Torres alipata wakati mgumu sana huku wengi wakifananisha usajili wake na ule wa Andriy Chevchenko mwaka 2006.


Torres ni mtu ambaye uwezo wake unafahamika na wachezaji wote wanaocheza ligi kuu ya England , akiwa amepata muda wa kutosha kwenye “pre-season” wa kujiandaa na kujiweka fit na pengine ujio wa kocha mpya Andre Villas Boas utampa nguvu mpya kwani mashabiki wa Chelsea wana hamu ya kumuona Fernando Torres wa zamani aliyewahi kuwatungua mara 8 kwenye mechi mbalimbali akiwa na Liverpool,


japo kuna kila dalili kuwa bado Villas Boas hajapata mfumo sahihi wa kumchezesha Torres na ishara zinaonyesha kuwa Torres ataanzia Benchi msimu utakapoanza hasa ukizingatia kuwa Chelsea imemsajili mshambuliaji mpya Romelu Lukaku.



Jack Rodwell (Everton)


Pamoja na umri wake mdogo wa miaka 20 tu , Rodwell ni mtu aliyeko kwenye hatua muhimu sana kwenye maisha yake kama mcheza soka . Kwa muda mrefu kijana huyu amehusishwa na uhamisho wa kwenda Manchester United lakini hivi karibuni Sir Alex Fergusson alichagua kumsajili Phil Jones baada ya Rodwell kuwa majeruhi kwa muda mrefu kwenye msimu uliopita.

Mwenyewe amekiri kuwa msimu wa mwaka 2011/12 utakuwa muhimu sana kwake . Rodwell alishindwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha Everton . Rodwell ana uwezo wa kucheza kwenye nafasi ya kiungo mkabaji japo anauwezo wa kupanda mbele pia au hata nafasi ya beki wa kati . Kama hatapata nafasi ambayo atatulia nayo kuna uwezekano mkubwa akajikuta akitumika kama mchezaji wa kujaza nafasi za wachezaji wengine wanapokosekana uwanjani .





Stewart Downing (Liverpool)



Ana kasi , ni mjanja , ana mguu wa kushoto wa hatari sana ,ana uwezo wa kufunga , kutengeneza mabao . Pengine timu nyingine hazitambui uwezo wake ila sisi tunaujua na ndio maana tumemsajili kwa kuwa ni mchezaji mwenye vitu vingi sana kiufundi na ndio tulichokuwa tunahitaji kwenye timu yetu”.

Hayo yalikuwa maneno ya mkurugenzi wa masuala ya soka kwenye klabu ya Liverpool Damiano Commoli ambaye hakusita kumsifia Stewart Downing baada ya kukamilisha usajili wake toka klabu ya Aston Villa. Maneno ya Commoli yanaweza kuonekana kuwa na chumvi iliyozidi kwa kuwa kila mtu anafahamu kuwa Downing hana uwezo na kasi inayohitajika kwa mawinga japo ana kipaji kisichopingika .

Unapokuwa na mtu kama Andy Carrol ni dhahiri kuwa unahitaji kuwa mawinga watakaomlisha krosi nyingi za ukweli, hiyo itakuwa kazi kubwa ya Stewart Downing kwenye timu ya Liverpool na kama akishindwa kuifanya basi watu hawatakuwa nyuma kuhoji paundi million 20 zilizotumika kumsajili.

Thamani yake kiukweli imeongezekan kutokana na ukweli kuwa ni raia wa England na mashabiki wengi ambao walikuwa wanahitaji kuona mchezaji kama Marko Mantin au Juan Mata watahitaji kudhihirishiwa thamani ya Stewart Downing .




Jonathan Woodgate (Stoke)



Jonathan Woodgate ni mtu ambaye ametumia muda wake mwingi akitibu majeraha mbalimbali , mara zote nne ambazo amewahi kuuzwa toka klabu moja kwenda nyingine amekuwa akiuzwa kwa thamni kubwa sana . Usajili wake wa mwisho unamshuhudia akisajiliwa na Stoke City kwa usajili wa bure .

Kwenye miaka yake miwili ya mwisho akiwa na Tottenham hotspurs Woodgate alicheza jumla ya mechi nne , na klabu ikaamua kutomuongeza mkataba . Akiwa na umri wa miaka 31 ni ajabu kuwa maisha yake katika soka la ngazi ya juu kama ligi kuu ya England bado hayajaisha , ila Tony Pulis ana imani kuwa maisha haya yanweza kurefushwa japo kidogo kwa kuzipa umuhimu siku za mechi kuliko mazoezi .

Tony Pulis amesema kuwa atajitahidi kumpa muda mfupi wa mazoezi na muda mrefu wa mechi ili kumuongeza muda wa kucheza kwa hali yake ya kiafya . Pullis anasema kuwa anaamini kuwa Stoke ina timu nzuri ya wataalamu wa afya. Inawezekana kuwa Tottenham timu yake ya zamani ina njia tofauti ya kufanya mambo ila kwetu ni tofauti na Woodgate atakuwa msaada kwetu .

Kama Tottenham walivyoweza kumchezesha Ledley King mchezaji mwingine mwenye majeraha sugu ya goti mechi 32 kwenye msimu uliopita basi hilo linawezekana pia kwa Stoke japo bado kuna wasiwasi mkubwa juu ya uwezo wa mwili wa Woodgate kuhimili mikikimikiki ya ligi kuu ya England . Kwa Tony Pulis , ana imani kuwa Woodgate anaweza kuwa moja ya usajili bora wa msimu .

Kama ilivyo kwa wengine kwenye orodha hii Woodgate naye anapaswa kutumia msimu huu kama nafasi yake ya mwisho ya kuwaonyesha watu kuwa miaka yote aliyopigana na majeraha mbalimbali ya goti haijaenda bure .

Jermain Defoe (Tottenham)



Umekuwa wakati mgumu sana kwa Jermaine Defoe . Akiwa amefunga mabao 18 kwenye ligi msimu wa mwaka 2009-10 , defoe alifunga mabao 4 tu msimu uliofuata . Majaliwa yake hayakusaidiwa na ukweli kuwa aliumia siku nne tu baada ya kufunga hat-trick kwenye mchezo baina ya England na Bulgaria mwezi septemba , lakini hata pale alipokuwa fiti Defoe hakufanya makubwa .

Mwezi mei Ddefoe alisema kuwa anaweza kulazimika kuondoka ikifikia hatua mbaya baada ya kuwa ameanza mechi 14 tu . Kocha wake Harry Redknapp alisema kuwa kama Defoe akicheza vyema atapangwa kama asipocheza vyema siwezi kumchagua kwenye timu .

Ukosefu wa mshambuliaji aliye kwenye fomu uliigharimu Spurs vibaya mno kwani wameshindwakurejea kwenye ligi ya mabingwa . Huku wakiwa na lengo la kurejea huko msimu ujao ni wakati wa Defoe kurudi kwenye kiwango chake au atajikuta anatafuta pa kwenda .




Mario Balotelli (Manchester City)



Baloteli ni mtu mwenye uwezo na kipaji kisichopingika . Cha ajabu ni kwamba badala ya kutengeneza vichwa vya habari kwa kutumia kipaji chake na kuiteka dunia kwa uwezo wake mkubwa Balotelli siku zote amekuwa akipamba vichwa vya habari kwa sababu mbaya .

Maisha yake ya soka yamejaa matatizo ya nje ya uwanja na wakati mwingine huwa analeta utata wake hata ndani ya uwanja .
Akiwa na Inter Milan , Balotelli aliwahi kutukanwa na kocha wake Jose Mourinho na wakati mwingine aliwahi kuchapwa makofi na mchezaji mwenzie Marco Materazzi kwa tabia yake chafu aliyoionyesha wakati wa mchezo dhidi ya Barcelona ;


Akiwa City Roberto Mancini alishindwa kuvumilia upuuzi wa Balotelli pale alipotolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa ligi ya Europa dhidi ya Dynamo Kyiv . Mwezi Aprili mwaka huu Silvio Berlusconi alitangaza kuwa ndoto ya Balotelli ya kuichezea timu anayoipenda ya Ac Milan haitotimia , kwa maneno yake mwenyewe Berlusconi alisema hivi “ kuna tabia ambayo watu wanaohusishwa na Ac Milan wanapaswa kuwa nayo na sidhani kama Balotelli yuko karibu na kuwa na tabia hiyo “.

Hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo mwehu Balotelli ameyafanya katika kipindi kifupi akiwa na Man city ila umefikia wakati way eye kujitambua kama mchezaji na kutambua kuwa Mancini amefikia hatua ya mwisho kwake na kama hatadhihirisha uwezo wake msimu huu basi huu unaweza kuwa mwanzo wa mwisho wake .




Anderson (Manchester United)



Japo bado ana umri wa miaka 23 , Anderson anajiandaa kuanza msimu wake wa tano akiwa Old Trafford . Fc Porto walilipwa euro million 20 wakati walipomuuza Anderson kwa Man United mwaka 2007 , na katika kipindi hicho Anderson ameonyesha ishara za thamani ya fedha zilizolipwa kwa ajili yake lakini bado hajawa na mwendelezo wa uwezo na kipaji chake yaani ‘consistency’ndani ya kikosi cha kwanza cha Man United .

Anderson alifika Old Traford akiwa na lengo la kucheza kama beki wa kushoto lakini amejikuta akiwa kiungo mkabaji kwa muda mrefu akiwa England , ambapo ameonyesha kiasi fulani cha uwezo wake lakini bado hajaweza kujihakikishia nafasi ya kudumu huku akihangaika na matatizo ya majeruhi ya muda mrefu .

Alipokuwa Ureno Anderson alionyesha kila sababu ya kuitwa mrithi wa Paul Scholes na sasa ambapo ‘maestro’ huyu wa midfield ya Man United akiwa amestaafu pengine ni wakati sahihi kwa Anderson kuingia na kuonyesha kile alichokiona Ferguson nchini ureno .


Matt Jarvis (Wolves)
Jarvis alicheza vizuri sana akiwa na Wolves msimu uliopita , alitwaa tuzo za mchezaji bora wa mashabiki na mchezaji bora kwa wachezaji wenzie kwa timu yake ya Wolves , na mwezi machi alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na timu ya taifa ya England alipocheza dakika 20 za mchezo wa kirafiki dhidi ya Ghana .

Pamoja na hayo kiwango chake kilishuka baada ya mchezo wake wa kwanza akiwa na England na alikaa benchi kwenye michezo miwili ya mwisho ya msimu kwa timu yake .Mick McCarthy alimzungumzia Matt Jarvis kuwa na tatizo la kukosa changamoto wakati msimu ukielekea mwisho ,

ameweza kuwapita mabeki wengi wa pembeni msimu huu na amewapa wakati mgumu sana lakini unapofika wakati kama huo unapaswa kupiga hatua kwa kuwa watu wanakuchukulia tofauti .

Ana mambo machache ya kudhihirisha kwa mashabiki wa Wolves lakini pia kama mchezaji wa timu ya taifa ya England na pia kama mtu aliyehisishwa na kuhamishwa na vilabu vikubwa , anao uhakika wa nafasi kwenye timu ya Wolves ila bado ana mengi ya kudhihirisha .

1 comment: