Kwa kurejesha kumbukumbu mara ya mwisho Manchester United ndio waliomaliza kama mabingwa wakiweka historia ya kutwaa ubingwa wa 19 ambao hatimaye uliwazidi mahasimu wao wa muda mrefu Liverpool .
Kwa bahati mbaya kwa mashabiki wa Manchester United huwezi kuzungumzia taji la 19 la ligi bila kurejea “dhahma” ya Wembley. Huku wengi wakiamini kuwa United watafuta makosa ya mwaka 2009 na kuwafunga mabingwa wa Hispania ambao wengi wanawatazama kama timu inayocheza soka bora kuliko timu zote kwenye historia ya mchezo huu , Manchester United walikumbana na kipigo cha mabao 3-1 na kumaliza msimu wao kwa machungu yasiyosahaulika.
Kwa wale wanaotazama mchezo wa soka kwa jicho la tatu , la nne mpaka la tano walitambua moja kwa moja kuwa kipigo ilichokipata United pale Wembley lazima kingekuwa na athari Fulani kwenye kikosi cha United kwa msimu uliofuata( yaani huu unaoanza kesho ).
Na ndiyo kilichotokea Sir Alex Fergusson hakupoteza muda kwenye shughuli ya usajili huku akili yake ikiwa kwenye kulipa kisasi kwa Barcelona kwa jinsi “walivyomtetemesha” pale Wembley .United walianza kwa kumsajili kipa ambaye ndiye atakayekuwa mrithi wa Edwin Van Der Sar ,
walimnasa Mhispania David De Gea toka Atletico Madrid , baada ya hapo United walikamilisha Usajili wa beki chipukizi Phil Jones halafu wakamaliza na Ashley Young . Baada ya hapo United wakaanza kupunguza idadi ya wachezaji ambapo John O’shea , Wesley Brown na Gabriel Obertan waliuzwa kwa Sunderland na Newcastle United .
United bado wanaonekana kuwa kwenye soko la usajili baada ya kauli ya mkurugenzi mtendaji David Gill kusema kuwa bado kuna nafasi moja ya kujaza . Nafasi hii ni nafasi ambayo imekuwa gumzo kwa karibu wakati wote wa mapumziko ya kabla ya msimu kuanza .
Kama utakuwa umetazama kwa makini De Gea , Ashley Young na Phil Jones wamekuja kuziba mapengo ya kina Van Der Saar, Gary Neville na Ryan Giggs atakayestaafu mwishoni kwa msimu ujao .
Lakini bado kuna nafasi ya Paul Scholes ambayo bado iko wazi . Hapo linakuja jina la Wesley Sneijder mtu ambaye amekuwa akihusishwa na kurithi nafasi ya Scholes hasa baada ya tetesi za kuwasajili kina Luka Modric na Samir Nasri kuisha kimya kimya.Msimu huu utakuwa wa maadiliko makubwa kwa United ambayo inakuja na sura mpya ikiwa na vijana wengi huku wakongwe wakiwa wameendelea kupungua taratibu .
Kwa upande mwingine Chelsea timu iliyomaliza msimu ikiwa nafasi ya pili ilimaliza kwa kumfukuza kocha wake Carlo Ancelotti na wakati timu zingine zikifanya usajili Chelsea “walisajili” kocha Andre Villas Boas”, kocha ambaye ametokea kuliteka soka la ulaya akiwa na kikosi chake cha Fc Porto .
Andre Villas Boas alianza wakati wake akiwa na Chelsea kwa habari mbaya za kumkosa kiungo muhimu wa Chelsea Michael Essien ambaye alipata jeraha baya la goti ambalo litamuweka nje ya dimba kwa zaidi ya miezi sita . Villas Boas alijibu pigo hilo kwa kumsajili kinda wa Barcelona Ariel Romeu .
Baada ya hapo Chelsea imemsajili Romelu Lukaku , mshambuliaji mwenye umri wa miaka 18 toka Anderletch ya Ubelgiji . Lukaku anatajwa kama Didier Drogba mpya . Inavyoonekana kuna kila dalili kuwa Chelsea bado hawajamaliza usajili kwani kuna jina la Luka Modric ambalo limekuwa likihusishwa na jezi za bluu za London kwa muda mrefu .
Andre Villas Boas ana kazi kubwa sana ya kufanya kwenye kikosi chake ch Chelsea . Hakuna nayejua kwanini amemsajili Romelu Lukaku ilhali anao watu kama Drogba , Anelka, Torres na Daniel Sturidge .
Sawa unaweza kusema kuwa kwa umri wa miaka 33 alio nao Drogba na mwenzie Anelka Villas Boas anatazama mbali zaidi ya walipo washmabuliaji hawa wawili lakini vipi kuhusu Sturidge mtu ambaye alidhihirisha uwezo wake kwa mabao aliyofunga akiwa na Bolton alikokuwa kwa mkopo msimu uliopita .
Una maana gani kwa kijana huyu unaposajili mshambuliaji mwenye umri sawa na wake (sturidge) yaani Lukaku tena kwa fedha nyingi namna hii . Suala linguine muhimu ambalo litakuwa tatizo kwa sasa kwa Boas ni mbinu ya kuwachezesha Drogba na Torres kwenye uwanja mmoja .
Tatizo kubwa la Chelsea halijawahi kuwa kocha , bali mmiliki wa timu Roman Abramovich ambaye hajawahi kuwapa makocha muda wanaohitaji kujenga timu na kama hataiacha tabia ya kuwaajiri na kuwafukuza basi ni dhahiri mafanikio atakuwa akiyasikia kwa timu zingine .
Washindi wa tatu kwenye msimu uliopita walikuwa Manchester City . Kuna vitu ambavyo timu hii inayomilikiwa na mabilionea wa kiarabu inacho kama Baraka na wakati huo kama laana .
Arsenal ambao kwa miaka ya hivi karibuni wametokea kuwa Academy ya Manchester City wana matatizo makubwa . Imepita misimu sita tangu washika bunduki watwae kombe lao la mwisho . Sababu zinazoinyima Arsenal makombe ni zile zile , kipa , beki na kiungo .
Mabingwa wa zamani Liverpool wameonekana kumaanisha biashara safari hii . Ukirudi nyuma wakati dirisha dogo la usajili lilipofunguliwa msimu uliopita King Kenny Dalglish alifanya usajili wa kumuuza Fernando Torres na kuwanunua Luis Suarez na Andy Caroll .
No comments:
Post a Comment