Search This Blog

Tuesday, August 2, 2011

Maisha baada ya Steven Gerard. Jinsi Liverpool walivyoweza kuishia baada ya kuondoka kwa nyota mbambali.

Maisha yatakuwaje Anfield baada ya kuondoka kwa Steven Gerard?
Hivi karibuni mashabiki wa Liverpool walipokea kwa mshtuko taarifa kuwa nahodha wao shujaa kama wanavyopenda kumuita “captain fantastic” atakosa mwanzo wa msimu wa ligi kuu ya England kwa majeraha ambayo kwa sasa yameanza kuwa sugu kwake huku yakitishia uchezaji wake wa muda mrefu.
Inawezekana umri umesogea sana au labda kucheza kwa muda mrefu bila kupumzika na wakati mwingine pia athari za muda mrefu za sindano za kuondoa maumivu pale alipokuwa akiumia siku za nyuma yoyote kati ya hayo ni sababu ila lililo dhahiri ni ukweli kuwa Steven Gerard hana muda mrefu wa kucheza kwenye kiwango cha juu na ni vyema Liverpool wakaanza kutafuta mbadala na ishara zote zinaonyesha kuwa Kenny Dalglish ameanza kufanya hivyo kwa kuwasajili kina Charlie Adam na Jordan Henderson na hata mwishoni mwa msimu uliopita chini ya Kenny Dalglish kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu Liverpool walionekana kucheza vyema bila Stevie G ambaye aliumia .
Historia inaonyesha kuwa Liverpool wameweza kufanikiwa kusonga mbele kwa mafanikio pale ambapo wachezaji tegemeo wanapokuwa wameondoka iwe ni kwa kustaafu au kuhama klabu na wafauatao ni baadhi ya watu ambao waliwahi kuwa tegemeo Liverpool na wakaondoka na Liverpool ikasonga mbele .
Billy Liddell


Kwa mashabiki wengi wa Liverpool ambao umri umesogea Billy Liddell ni mchezaji bora kuliko wote waliowahi kuchezea klabu hiyo . Liddell alicheza mechi takribani 534 ndani ya uzi wa Liverpool. Winga huyu toka Scotland alifunga mabao 228 katika kipindi cha miaka ya 1946 na 1960 . Katika kipindi cha miaka ya 1950 Billy Liddell alikuwa tegemeo la liverpool pale ambapo klabu hiyo iliyumba . Liddell alionyesha kuwa yeye ni Liverpool damu pale ambapo alibakia na klabu hiyo iliposhuka daraja mwaka 1954 baada ya kuwa wametwaa ubingwa mwaka 1947. Billy alikuwepo kwenye kipindi cha kocha mwenye mafanikio kuliko wote Liverpool Billy Shankly mwaka 1959 lakini hakukaa muda mrefu kwani alicheza mechi yake ya mwisho mwaka mmoja kabla mapinduzi ya Shankly hayajaanza.
Liverpool walichezaje baada ya Billy Liddell kuondoka? Kocha Bill Shankly alitambua kuwa Liverpool ni tegemezi kwa wajina wake Billy Liddell na aliona mbali kuwa wangepata tabu akikosekana hivyo alianza kujiandaa mapema na muda mfupi kabla Liddell hajaondoka rasmi Shankly alimpa nafasi chipukizi mwenye miaka 18Ian Callaghan kwenye kikosi cha kwanza . Callagan alianza taratibu lakini mwisho wa siku alikuja kuvunja rekodi ya mechi nyingi iliyowekwa na Billy Liddell mtu aliyekuwa akicheza kama mrithi wake ambapo Callagan alicheza mechi 857 akitwaa mataji mbalimbali England katika kipindi cha miaka 18.

Kevin Keegan



Kevin Keegan ni mmoja kati ya wachezaji wenye heshima kubwa Liverpool . Keegan alikuwa kwenye timu ya pili iliyotengenezwa na Billy Shankly ambapo alikuwa mmoja kati ya wachezaji maarufu duniani kwenye miaka ya sabini na ni yeye aliyeisaidia Liverpool kutwaa taji lao la kwanza la ulaya mwaka 1977 . Pamoja na taji hilo Keegan aliibeba liverpool kwenye ligi ya England ambapo Liverpool walikuwa mabingwa kwenye miaka ya 1973,76 na 77 sambamba na kombe la FA mwaka 1974, kombe la UEFA mwaka 1973 na mwaka 76 . Mashabiki wa Liverpool walipata presha waliposikia taarifa kuwa shujaa wao KK alikuwa mbioni kujiunga na Hamburg ya Ujerumani mwaka 1977.
Alipoondoka Keegan? Kocha wa Liverpool wakati Kevin Keegan anaondoka alikuwa Bob Paisley . Alichofanya Paisley kama hatua ya kuziba ufa ulioachwa na Kevin Keegan ni kulipa ada iliyokuwa rekodi kwa Liverpool ya paundi 440,000 kumsaini mshambuliaji Kenny Dalglish toka Glasgow Celtics . Dalglish alipewa jezi namba 7 aliyokuwa akiivaa Keegan . Huku namba 7 wa zamani wa Liverpool akifanya vitu vya hatari huko Ujerumani ambapo alitunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya kwa miaka ya 1978 na 79 , Liverpool hawakumkosa nyota huyo kwani namba 7 mpya Kenny aliiwasahaulisha mashabiki wa Liverpool kuhusu Kevin Keegan . Dalglish alianza msimu wake wa kwanza Liverpool kwa mafanikio makubwa na bao lake ndio liliipa Liverpool ubingwa wa ulaya kwa msimu huo na aliendelea na moto huo huo na aliishia kuwa mchezaji bora wa Liverpool mpya kwa miaka iliyofuata .

Graeme Souness

Kiungo huyo mwenye kupiga “tackling” za nguvu aliing’aa kwenye midfield ya Liverpool kwa miaka 6 tangu mwaka 1978 hadi 84, katika kipindi hicho Souness alitwaa taji kila mwaka katika miaka yote hiyo aliyocheza na mara nyingi ilikuwa ni taji zaidi ya moja . Souness aliondoka Liverpool 1984 baada ya kuiongoza Liverpool kama nahodha wake kutwaa ubingwa wa ulaya , ubingwa wa ligi ya England na ubingwa wa kombe la Ligi .
Liverpool waliishi vipi baada ya Souness ?
Muda mfupi kabla Graeme Souness hajaondoka Anfield Liverpool ilimsajili kiungo John Wark na kwenye msimu wake wa kwanza Wark alifanikiwa kuwa mfungaji bora akiwa na mabao 27 kwenye mashindano yote . Kwenye msimu wake wa pili John Wark aliweza kutwaa mataji mawili lakini mchango wake ulikatishwa na majerha aliyoyapata msimu huo na ujio wa wachezaji wawili Jan Molby na Steve McMahon kama wapinzani wake kwenye midfield ya Liverpool . Hadi nusu ya kwanza ya ligi ya mwaka 1987/88 inaisha John Wark alikuwa njiani kurudi kwenye klabu yake ya zamani Ipswich Town. Na hapo Liverpool walikuwa wameziba nyufa mbili kwa wakati mmoja ufa wa Graeme Souness na wa John Wark .


Alan Hansen

Katika mechi 620 alizoichezea Liverpool kati ya miaka ya 1977 na 1991 Alan Hansen alileta ladha tofauti kwenye safu ya ulinzi ya Liverpool . Staili yake ya uchezaji ambayo ilikuwa tofauti na mabeki wa uingereza ambao hupenda ‘butua butua’ ilimpa Hansen Upekee. Jamaa alikuwa akiwapokonya washambuliaji mpira na kuundoa kwenye eneo la hatari kwa umakini wa hali ya juu na alikuwa mmoja wa watu walioipa Liverpool mafanikio makubwa katika kipinndi chake msimu hadi msimu kwa miaka yote 14 aliyoichezea Liverpool . Hansen alitwaa mataji 8,na alikuwa nahodha wa Liverpool wakati walipotwaa mataji mawili mwaka 1986 .
Liverpool waliziba vipi pengo la Hansen? Wakati Hansen alipostaafu mwaka 1991 kocha wa Liverpool Graeme Souness alitumia paundi milioni 2.2 kumsajili beki wa timu ya taifa ya England na Derby County Mark Wright kuziba pengo lake . MarimWright alikumbwa na balaa la majeruhi alipoojiunga na Liverpool. Ila Wright alitwaa kombe la FA kama nahodha wa Liverpool kwenye msimu wake wa kwanza . Wakati wa Souness kama kocha wa Liverpool uligubikwa na timu mbovu ambayo ilishindwa kufanya vyema kama Liverpool za miaka iliyopita ila pamoja na hayo Mark Wright alikuwa mchezaji wa kipekee . Hilo lilidhihirika pale aliposhutumiwa kuwa mchezaji mbovu na kocha wa zamani wa Liverpool Roy Evans , Wright alirejea kwenye kiwango chake katika kipindi ambapo Liverpool walionekana kufufuka na kurejea kwenye enzi zao katikati ya miaka ya 90. Jumla ya mechi 210 akiwa na jezi nyekundu za Liverpool zilimpa Mark Wright heshima aliyostahili kama gwiji wa Anfield lakini ukweli unabakia kuwa kwa mchezaji wa daraja na kiwango kama cha Mark Wright wakati wake na Liverpool ulikuwa mbaya sana kwake na kwa klabu ya Liverpool.

No comments:

Post a Comment