Raisi wa TFF-Leodegar Tenga.
Na Shaffih Dauda Blogger
Kuboreshwa kwa kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi ambapo imeongeza Kamati mpya ya Ligi itakayokuwa inafanya kazi za Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo kumeelezwa hakuna tija yoyote.
Akizungumza kwenye kipindi cha Sports Round Up cha kila wiki, Mchambuzi nguli wa masuala ya michezo nchini Shaffih Dauda amesema hilo linajitokeza kutokana na takwimu za nyuma za TFF.
Hivi karibuni Rais wa TFF, Leodeger Tenga alisema kamati hiyo ya ligi itaundwa ili kuipunguzia mzigo Kamati ya Mashindano."Kamati hiyo itaundwa na baadhi ya watu wanaotokea katika klabu, lengo ni kuipunguzia kazi Kamati ya Mashindano," alisema Tenga.
Mbali ya kamati hiyo, Tenga alisema msimu ujao kila klabu ya Ligi Kuu, kabla ya kuanza kwa mashindano inatakiwa kuhakikisha inafanyia mahesabu yake ya msimu uliopita, kwa sababu tayari kila klabu inawatunza fedha wake wa kuajiriwa.
Kutokana na kauli hiyo mchambuzi huyo amesema kwa jinsi mfumo wa uendeshaji Ligi ulivyo kamati hiyo haiwezi kufikia malengo yake hali inayochangiwa na muundo mzima watendaji wa kamati hiyo.
“Kamati yote ya watendaji washiriki wake wanachaguliwa na Rais wa TFF na vilabu ambavyo ndivyo wamiliki wakuu wa ligi hiyo hawahusishwi wala kuchagua wajumbe wa kamati hiyo,” alisema Dauda.
Kwa upande wake Mchezaji Mstaafu wa klabu ya Yanga ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji wa timu hiyo Ally Mayay alisema soka la Tanzania linahitaji mabadiliko ya kweli kufikia soka la kimataifa na linaloendana na ushindani.
“Waraka wa TFF unaelekeza uwepo wa watendaji watatu kwenye kamati hiyo kutoka vilabu vya ligi kuu. Kimsingi naona hilo halijazingatiwa na ndicho kitu kitakachoiangusha kamati hiyo ya Ligi,” alisema Mayay.
Akiongeza Dauda kamati zote zilizopo nchini zimeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo na kuonesha mapungufu. Kutokana na hilo kinachotakiwa ili Tanzania iweze kufanya vizuri katika medani ya mpira ni kuajiri wataalam wenye sifa zao.
Akilifafanua hilo mmiliki wa Klabu ya African Lion Rahim Zamunda amesema watalaam kutoka nje wataleta maendeleo na itakuwepo fursa ya kuondolewa pale atakaposhindwa kufanya kile kinachotarajiwa.
“Mfano ni huu, nchini kuna timu 14 zinazoshiriki lgi kuu ya Bara, lakini watendaji wake bado wanaoonekana kutokuwa na umoja wa kuleta mabadiliko ya kisoka nchini. Jana tuliitwa kwa mkutano wa wamiliki wa vilabu saa sita mchana lakini hadi kufikia saa 8 mchana ni wamiliki sita tu ndio tuliohudhuria na mkutano ukaahirishwa,” alishangaa Zamunda.
Kutokana na mfumo huo Mmiliki wa African Lion amesema yanahitajika mageuzi makubwa yatakayochangia wadhamini kutoka taasisi mbalimbali kudhamini ligi au vilabu vya soka.
“Kama mpira unatakiwa kuzalisha, hivyo unatakiwa uendeshwe kibiashara kwani hakuna mtu anayetaka kufanya kitu ambacho kinampotezea fedha badala ya kumuingizia hata kama ni mpenzi kwa kiasi gani,” anaeleza Zamunda.
Tofauti na hilo mmiliki huyo ametishia kutovaa jezi za wadhamini wa ligi kuu nchini mwakani mpaka pale atakapolipwa fedha zake za ushindi iliyopata timu yake baada ya kuwa timu bora yenye nidhamu misimu miwili iliyopita.
Zamunda anasema hadi sasa anaidai TFF Milioni 5.5/- na hajalipwa mpaka sasa. Mimi ni mfanyakazi wa Push Mobile, lakini nilipotaka timu yangu waiunge mkono kampuni yangu walikataa, sasa kuna maslahi gani kuwa na mdhamni ambaye hamfaidiki na matunda yake? Alihoji.
“Sisi hatuvaa jezi za mdhamini wa ligi kuu kwani hatujui mkataba ukoje, tukiwa kama washiriki au mmoja wa wamiliki wa timu iliyo kwenye ligi kuu sijawahi kuona mkataba kati ya TFF na klabu wala kuitwa kwenye vikao vya maamuzi”.
“Wamiliki ni sawa na Body Members, kwa hiyo wanatakiwa kufanya kazi karibu na watendaji wa TFF ili kuunda muundo unaoeleweka wa ligi. Kwa mfumo huu Tanzania inapoteza pesa nyingi kwa kukosa udhamini bora kwenye ligi kama zilivyo nchi za Kenya na Uganda ambazo tayari zinanufaika baada ya kufanya maamuzi kwenye muundo wa uongozi,” anabainisha.
No comments:
Post a Comment