Wakati msimu mpya wa ligi mbali mbali barani ulaya ukitaraji kuanza ,Watu wengi hawawezi kuisahau mechi ya fainali ya Uefa Champions League ya msimu uliopita kati ya Man utd na Fc Barcelona. Ndiyo, ilichezwa katika kipindi cha majira ya joto barani Ulaya katika uwanja wa Wembley jijini London. Ni nani anaweza kusahau balaa la Barcelona dhidi ya Manchester United.
Mwisho wa siku, ilikuwa ni mechi iliyozikutanisha timu mbili bingwa kutoka Ligi mbili bora zaidi duniani kwa sasa, Ligi Kuu ya England ‘Premier league’ dhidi ya ligi kuu ya Hispania, Primera League.
Manchester ilipotezwa uwanjani na wachezaji wake wakajikuta wakifukuza vivuli vya wachezaji wa Barcelona. Lakini je, ni kweli pambano moja linaweza kuamua ubishi uliotanda nchini kuhusu ligi bora duniani kati ya ile ya England dhidi ya Hispania?
Mashabiki wengi wa soka nchini wamekuwa wakibishana kuhusu ipi Ligi bora baina ya hizi mbili. Ukweli ni kwamba hakuna Ligi bora baina ya hizi mbili, inategemea tu shabiki anategemea aina gani ya soka.
Kuna wale wote ambao wanapenda zaidi staili ya soka la nguvu, kasi na hamasa iliyopindukia. Kwao watalipenda zaidi soka la Uingereza kuliko soka la Hispania.
Kuna wale ambao wanalipenda zaidi soka la kitabuni, soka lisilotumia matumizi makubwa ya nguvu wala kasi isiyo na sababu. Hawa watalipenda zaidi soka la Hispania kuliko soka la Uingereza. Na ndiyo maana mashabiki duniani wamegawanyika katika pande kuu mbili.
Kwa Uingereza, ushindi ni zaidi ya kucheza soka maridadi. Ni zaidi ya kupiga kanzu, tobo, chenga za maudhi na mbwembwe nyingine uwanjani. Wanachotaka ni ushindi tu na soka la kazi.
Kocha maarufu wa zamani wa Liverpool, Billy Shankly aliwahi kusema; “Kuna watu wanaosema soka ni mchezo wa maisha na kifo, mimi naona ni zaidi ya hapo”. Bill alikuwa anawakilisha falsafa ya soka la Kiingereza.
Kwa Hispania, soka si hivyo. Soka ni mchezo maridadi wa kuonyeshana ubora uwanjani na si vinginevyo. Kwao, bao maridadi linasakwa kwa mbinu maridadi na si zile za Kiingereza za kulazimisha zaidi.
Jaribu kutazama wakati timu ya Kiingereza inapojaribu kutafuta bao la kusawazisha. Soka litakalochezwa hapo ni la mipira mirefu, krosi, kona na kila mbinu ya ushindi wa haraka haraka. Kwa Hispania, soka litakalochezwa ni lile la kumiliki zaidi mipira na kutafuta mbinu za kupenyeza mipira ya chini katika misitu ya walinzi wa timu pinzani.
Na hapa ndipo linapoibuka jibu la kwa nini wachezaji wengi wa bara la Amerika Kusini wanapenda kucheza Ligi kuu ya Hispania kuliko ligi kuu ya England. Ligi kuu ya Hispania ni ndoto yao kwa sababu inafiti mfumo wao wa uchezaji kuliko Ligi kuu ya England.
Amerika Kusini, katika nchi kama Brazil, Argentina, Paraguay, Chile na nyinginezo, soka linachezwa katika staili ya kumiliki mpira zaidi na kuonyesha vipaji binafsi tofauti na Uingereza.
Kuanzia enzi za akina Diego Maradona, Romario, Careca, Rivaldo na wengineo, mpaka enzi hizi za akina Lionel Messi, Diego Forlan, Ronaldinho na wengineo, wachezaji wa Amerika Kusini wametamba zaidi Hispania na hata Italia, kuliko Uingereza.
Na wakati mwingine unaweza pia kupima namna ambavyo wachezaji wengi wa Hispania, au waliowahi kucheza Ligi ya Hispania namna walivyoshindwa kung’ara katika soka la Kiingereza.
Akina Josemi, Fernando Morientes, Asier del Horno, Maxi Rodriguez, Patrick Kluivert, Davor Suker na wengineo wengi kutoka Ligi Kuu ya Hispania walichemsha kucheza katika kiwango cha juu katika Ligi Kuu ya England.
Kasi na nguvu za soka la Uingereza ziliwashinda. Wakati wao wakifikiria zaidi kukaa na mipira na kucheza kwa uhuru, Ligi ya Kiingereza ilihitaji zaidi wachezaji wanaocheza kwa haraka na kuvamiana bila ya kuhitaji mipango sahihi ya soka.
Shukrani kwa Fernando Torres, Claude Makelele na Xabi Alonso ambao walimudu kwa kiasi kikubwa kasi ya ligi kuu ya England. Siwezi kumzungumzia Cesc Fabregas kwa sababu aliingia staili ya soka la Uingereza akiwa kinda na imempa wakati mzuri wa kuijulia kwa ufasaha.
Lakini rekodi zinaonyesha wachezaji wengi wanaotoka Ligi Kuu ya Uingereza kwenda Hispania, huwa hawapati mgumu wa kumudu soka la Kihispania. Sababu kubwa ni kwamba wanajikuta wakiwa katika nafasi nzuri ya matumizi ya nguvu kuliko wachezaji waliowakuta.
Wakati Michael Owen akionekana ameanza kusuasua katika Ligi Kuu ya Uingereza, Liverpool ilimtia sokoni. Lakini akaibuka na mabao 13 ya Ligi katika Ligi ya Hispania wakati rekodi yake ya ufungaji msimu mmoja kabla pale Uingereza ikionekana kuwa finyu.
David Beckham, Nicolas Anelka ‘Le Sulk’, Ruud Van Nisterlooy, Diego Forlan na wengineo wameonekana kuingia moja kwa moja katika mfumo wa uchezaji wa Hispania bila ya shida.
Msimu mmoja baada ya Sir Alex Ferguson kumuuza Diego Forlan, nyota huyo wa Amerika Kusini aliibuka kuwa mmoja kati ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Hispania. Uingereza alionekana kama vile ni mshambuliaji wa kawaida.
Wengine wanapima ubora wa Ligi kutokana na mafanikio yao katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya. Lakini hata wale ambao wanaamini kuwa Ligi Kuu ya England ni bora kuliko ile ya Hispania kutokana na mafanikio ya sasa ya timu za England za England katika michuano ya Ulaya, nadhani wanakosea kwa sababu tayari timu za Hispania zilishafanya mambo makubwa siku za nyuma.
Ni kweli Waingereza wametesa zama hizi, ikiwemo fainali ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Chelsea na Manchester United mwaka 2008 pale Moscow, Urusi. Lakini mwanzoni mwa miaka ya 2000 ni Hispania ndiyo ambayo ilitesa vilivyo katika soka la mabingwa wa Ulaya. Nao pia waliwahi kuingiza fainali ya timu mbili za Hispania kati ya Real Madrid na Valencia mwaka 2002.
Kwa kuhitimisha tu, nadhani ni wakati wa watu kuelewa kuwa linapokuja suala la timu ligi ipi ni bora kati ya England na ile ya Hispania, kigezo kinachoweza kutumiwa si mafanikio wala kingine zaidi ya mtazamo wa shabiki binafsi kuhusu staili ya soka analolipenda.
Kama utapenda soka la nguvu, kasi na vurugu za hapa na pale, nadhani soka la Uingereza litakaa moyoni mwako. Kama utapenda soka la akili zaidi, maarifa na ustaarabu wa kupeana nafasi katika kucheza soka, ni lazima utapenda soka la Hispania.
Bahati mbaya, FIFA hawana utaratibu wa kuchagua Ligi bora kama wanavyochagua wachezaji bora. Nadhani wako sahihi. Kinachobakia ni mtazamo binafsi wa shabiki kuhusu staili ya soka wanalolipenda. Kama vile wachezaji wa Amerika Kusini wanavyochagua…
No comments:
Post a Comment