Mabingwa wa soka Tanzania bara wanaingia uwanjani leo kuijaribu kuwafuata wenzao wa
Simba ambao jana walitangulia kufuzu kwa nusu fainali baada ya kuwafunga Bunamwaya
toka Uganda kwa mabao mawili kwa moja . Yanga wanacheza na Red Sea toka Eritrea na kwa mawazo ya haraka unaweza kufikiri kuwa huu utakuwa mchezo rahisi kwa mabingwa hawa wa soka Tanzania bara , lakini huu mpira bwana na kama wasemavyo wahenga mpira unadunda na hii inamaanisha kuwa lolote linaweza kutokea Yanga wanaweza kupoteza kama ambavyo wanaweza kushinda .
Ni muhimu kuutazama mchezo huu dhidi ya Red Sea kwa kutupia jicho yaliyotokea kwenye michezo mitatu ya Yanga na katika michezo mine ya Red Sea . Yanga wanaonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji ambayo inasaidiwa sana na safu nzuri pia ya kiungo ambayo inaonekana kuwa safi chini ya Rashid Gumbo na Nurdin Bakari huku Julius Mrope akisumbua san upande wa kulia na Kigi makassy akifanya mambo yake kwenye upande wa kushoto .Kenneth Asamoah , Davis Mwape na Hamis Kiiza wameonekana kuwa wasumbufu sana kwa safu mbalimbali za ulinzi kwa uwezo wao wa kujipanga na kuchachafya huku wakitumia nguvu na akili inapotakiwa na hadi kufikia mchezo dhidi ya Red Sea Yanga wameshafunga nane huku wakiwa na wastani wa angalau mabao mawili kila mechi huku Hamis Kiiza na Davis Mwape wakiwa wameshatupia bao mbili kila mmoja na kuna kila sababu ya kuamini kuwa wana uwezo wa kuongeza mabao hayo kwenye mchezo dhidi ya Red Sea .
Tatizo moja kwa Yanga limeonekana kuwa kwenye eneo la ulinzi ambapo pamoja na mabao nane ambayo yanga imeyafunga kwenye imeruhusu nusu ya idadi ya mabao hayo. Hii inamaanisha kuwa yanga imeruhusu wastani wa angalau bao moja kila mechi na hii ni hatari kwa kwa sababu siku ambapo Yanga itakutana na timu ambayo ina walinzi wenye nidhamu na kipa aliye na ubora hali inaweza kuwa ngumu . Red Sea inaweza kuwa timu ya aina hii , tazama jinsi walivyoweza kuwazuia Simba na kumaliza mchezo bila wavu wao kutikiswa na hapo utaona hatari ambayo Yanga wanaweza kukutana nayo .
Red Sea kwa upande wao wamecheza michezo mine ambapo ambapo wameza kushinda michezo miwili wakishinda moja bila dhidi ya Vital’O, na mchezo mwingine wakishinda kwa mabao 4-1 dhidi ya Enticelles ya Rwanda na wamefungwa mchezo mmoja na Zanzibar OceanView ambao walifungwa mabao 2-0 na wametoka sare ya bila kufungana na Simba . Ukitazama matokeo hayo utagundua kuwa Red Sea wako kama Yanga kwa sababu wamefunga mabao matano na wameruhusu wavu wao kuguswa mara tatu huku wakicheza michezo miwili ambapo walikomaa na kuondoka na “Clean Sheet” .
Matokeo haya yanaonyesha kuwa Yanga hawapaswi kuwadharau Red Sea kwa sababu wameonyesha kuwa hawatabiriki , hujui utgemee lini toka kwao kwa sababu mashabiki wengi ambao walishuhudia Red Sea ikifungwa na Ocean View walitaraji kuwa Simba wangewamaliza kabisa lakini haikuwa hivyo na hata kwenye ufungaji wanaonekana wanao uwezo wa kufunga hivyo kama ngome ya Ynga iliyoko chini ya kina Canavarro na Chacha Marwa , Godfery Taita na Shadrack Nsajigwa na wakati mwingine Oscar Joshua haitajipanga vyema maajabu yanaweza kutokea ila kwa waliowatazama Red Sea kwa jicho la tatu hawatashangaa kwa sababu wameshaona ishara zote za hilo kutokea .
Yaw Berko golikipa namba moja wa Yanga ni kipa imara ambaye huwapa mashabiki uhakika wa asilimia mia moja na hamsini awapo golini kwa ustadi wake na uweoz wake mkubwa wa kudaka hata pale kwenye zile “one-on-one situation” lakini kama ilivyo kwa kipa yoyote ulimwenguni kuna vipindi ambapo mabeki wake hawampi ulinzi wa kutosha na ndio maana hadi leo ameruhusu wavu wake uguswe mara zisizopungua nne .
Hii ni hatua ya mtoano ambapo baada ya dakika tisini matokeo yakiwa sare mwamuzi ni penati na kwa aina ya mchezo ambao Red Sea wanaucheza usishangae wakaiingia na mtazamo wa kutafuta sare huku wakilenga matuta ili wawashangaze wapinzani wao ambao uenyeji wao unawapa ‘edge’ muhimu ya kushinda .
Mi vyema Yanga wakaamua kulinda kiukweli kwenye mchezo wa leo , Cannavaro na Chacha ambao ni wakabaji wazuri ila miongoni mwao hakuna wa kumuongoza mwenzie hali inayosababisha wakatike mara kwa mara na wakati mwingine kuchanganyana na kumwacha adui apite katikati yao kama ilivyokuwa kwenye mcezo wa kwanza dhidi ya El Mereikh , pia Taita na Nsajigwa wana kawaida ya kupandisha mashambulizi na kujisahau na kukamatwa kwenye ‘counter-attack” . Pia kama akicheza , Oscar Joshua ana kawaida ya kutumia nguvu nyingi kuliko maarifa hali ambayo vijana wa Red Sea wanaweza kuitumia na kuanza kujiangusha na kumtafutia kadi ambayo itaidhuru Yanga .
Kama safu ya ulinzi ya Yanga ikicheza kwa mipango na kwa nidhamu basi Yanga wana walau asilimia 75 ya uhakika wa kushinda kwa sababu kwenye ushambuliaji hawana matatizo mengi .
No comments:
Post a Comment