Yanga.
1. Yaw Berko
Hakusumbuliwa sana kwa sababu washambuliaji wa Simba mara nyingi hawakupeleka mipira ambayo ingembugudhi na kumpa wasiwasi kama ile ambayo yanga walipeleka kwenye lango la Simba.( 7/10 )
2.Shadrack Nsajigwa .
Kama ilivyo kawaida yake , alikuwa akiongoza kwa mfano , “work ethic” yake ilikuwa juu, na hakupata tabu kuwamudu viungo wa Simba na alipata wakati mwepesi kumkaba Salum Machaku ambaye hakuwa na ujanja wa kumpita . ( 7/10 )
3.Oscar Joshua .
Kwa nguvu nyingi alizokuwa anatumia ungeweza kudhani kuwa angeigharimu timu yake lakini haikuwa hivyo kwani ali-win “Battles” nyingi sana na viungo wa Simba na haishangazi kuona kuwa upande wake ulikuwa salama kwa muda mrefu wa mchezo.( 7/10 )
4.Nadir Haroub Cannavaro.
Alikuwa kwenye kiwango chake cha siku zote ambapo alikuwa anatumia nguvu na akili pale inapohitajika, na jinsi mchezo ulivyokuwa kwa ujumla ulikuwa unampa wakati mwepesi kazini japo alionyesha “lack of professionalism” kwa kumchokoza Haruna Moshi ili kumtafutia kadi , pia alikuwa na wakati ambao tatizo lake kubwa ambalo ni kukosa mawasiliano na mabeki wenzie lilionekana na lingeweza kuidhuru timu yake . ( 8/10 )
5.Chacha Marwa.
Alicheza kwa ujasiri mkubwa kama ambavyo ametokea kuwa mtu wa kutegemewa kwenye “kumi na nane” ya Yanga . Hakuwa na papara sana na wala tatizo la kukosa mawasiliano baina yake na beki mwenzie wa kati Cannavaro halikuonekana sana na halikuonekana kwa sababu yake. ( 7/10 )
6.Nurdin Bakari.
Kama kuna mtu ambaye alikuwa nyota wa mchezo tena kwa alama zote basi Nurdin anaqualify kuwa mtu huyo , alikuwa ana-enjoy kucheza soka na alikuwa akifanya mambo bila papara ambazo wachezaji wanakuwa nazo wakati wa mechi kubwa kama hii , alikuwa na uhuru mwingi sana eneo la kati kati ya uwanja . Kuna mambo makuu matatu ambayo yalimsaidia Nurdin , kukosekana kwa Jerry Santo, kutoka mapema kwa Mwinyi Kazimoto na pia kuwa nje ya mchezo kwa aliyeingia kuchukua nafasi ya Mwinyi, Mohamed Banka ambaye mchezo wake uliokosa mwelekeo na malengo ulimpa faida kubwa Nurdin bakari.( 9/10 )
7.Godfrey Taita.
Kwa upande wake kidogo alikuwa anakosa maarifa ya kumkabili Amir Maftah ambaye mara nyingi huwa ana tatizo la kukosa umakini kwenye kukaba , hakuwa na madhara mengi kwa beki ya Simba na krosi zake zilikuwa haziongei kwa maana ya kuwa na madhara kwa mpinzani na kuwa na faida kwa washambuliaji wake aliokuwa anawalisha. Kama walinzi wengi tulio nao kweye nafasi yake alikuwa anatumia nguvu nyingi kuliko maarifa labda ni kutokana na kuzoea kucheza kwenye defence mara kwa mara na pia yawezekana alikua na fatigue baada yak kucheza dakika 120 za nguvu kwenye mchezo wa nusu fainali. ( 6/10 )
8.Juma Seif Kijiko .
Hakuna aliyekuwa anajua mengi kuhusu mchezaji huyu kabla ya michuano hii japo alikuwepo Yanga na alicheza baadhi ya mechi za ligi kuu msimu uliopita na nyingi alikuwa benchi . Ameleta aina tofauti ya mchezo ambao haupo Yanga , ana uwezo mkubwa wa kumiliki mipira kwa kujiamini kwa hali ya juu na ni dhahiri kwamba kama asingeumia basi pengine Rashid Gumbo asingeingia kwa sababu kabla ya hapo hakuna mengi aliyoyafanya ambayo ungeyaita makosa alikuwa akiuficha mpira vizuri na kwa uhakika wa hali ya juu sana na alikuwa akitoa challenge kubwa kwa viungo wa Simba ambao walikuwa wakimiliki sana mipira . ( 7/10 )
9.Davis Mwape .
Mwape ni mshambuliaji asilia , mtu mwenye nguvu nyingi na ni mjasiri asiyekata tamaa, tatizo kubwa ambalo Yanga wameendelea kulifanya juu ya mchezaji huyu ni kutocheza kwa ajili yake . Kwenye mchezo dhidi ya Simba Mwape alicheza nje ya eneo la kumi na nane na hapa huwezi kuona madhara yake kwa mpinzani japo kuna nyakati ambazo alikuwa akiwatisha mabeki wa Simba hasa kwa mipira ya krosi lakini tofauti na hapo ni kama hakuwepo mchezoni na siku ambayo Yanga watagundua njia ya kumchezesha Mwape basi watakuwa wanafunga magoli engi sana na si kumlazimisha acheze nafasi ambayo analazimika kudrible wakati hiyo si kazi yake aliyozaliwa kufanya uwanjani . pia ‘work rate’ yake ilikua juu mno. ( 7/10 )
10.Jerry Tegete .
Kama ilivyo Mwape Tegete alikuwa anachezeshwa “out of position” na alijitahidi kwa kiasi kikubwa sana ku-adopt kwa jukumu alilopewa na alikuwa akiwatoa mabeki wa Simba nje ya eneo na kutengeneza mashimo ambayo kama Yanga wangekuwa makini yangekuwa mashimo ambayo yangewapa magoli mengi . Kimsingi Tegete ni mtu ambaye anapaswa kutumia akili nyingi sana kuwavizia wapinzani na kutafuta njia ya kufunga na si kutafuta njia ya kuwaondoa mabeki nje ya eneo ( withdrawn position ) japo kwa jukumu alilopewa alilifanya kwa ukamilifu .( 8/10 )
11.Kiiza Hamis .
Kiiza ni mchezaji mjanja sana maybe muda wowote anaweza kufanya kitu chenye faida kwa timu yake , ukiacha Nurdin Bakari Kiiza ni mtu ambaye aliwasumbua sana Simba na alikuwa anahaha uwanja mzima kutafuta nafasi na kupenyeza mipira kwa wenzie , pengine mchezo usingekuwa kama ulivyokuwa kama asingekuwepo . alifunga bao ambalo sidhani kama kweli alikua ameotea. ( 7/10 )
Walioingia .
12.Rashid gumbo .
Ni kama alikuwa na deni la kuwalipa Yanga na wakati huo huo alikuwa na kisasi cha kuwalipizia Simba , alimiliki sana mipira eneo lake la katikati ya uwanja na alirejesha “partnership” na Nurdin na kilichomongezea alama kwenye mchezo wa fainali ni krosi yake ambayo ilikutana vyema na kichwa cha Keneth Asamoah ambaye aliukwamisha mpira wavuni na kuipa Yanga ubingwa . ( 7/10 )
13.Keneth Asamoah.
Aliingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete ambaye alitoka wakati wa muda wa nyongeza. Kwa wale waliodhani kuwa Asamoah ni garasa ambalo Yanga imekula hasara kulisajili basi Asamoah amewajibu kwa njia bora ya goli safi ambalo bila shaka limemaliza ubishi wake. ( 7/10 )
Jullius Mrope .
14.Aliingia kuchukua nafasi ya Godfrey Taita na hakuleta “impact” kubwa kwa sababu hakumpa tabu Amir Maftah kwenye upande wake na kilichomuokoa ni ushindi ambao Yanga iliupata. ( 6/10 )
Kocha , Sam Timbe .
Falsafa yake ya kucheza soka la matokeo zaidi imeonekana kuinufaisha Yanga na amefaulu kuandika historia ya kipekee kwa kutwaa ndoo akiwa na timu ya nne , soka lake la moja kwa moja ambalo lina madhara kwa mpinzani limeonekana leo na ndio limeipa Yanga ubingwa na anakuwa kocha gwiji wa michuano na ukanda huu wa Cecafa.
Walivyocheza Wachezaji wa Simba.
1.Juma Kaseja.
Alisimama vizuri langoni japo walinzi wake hasa mlinzi wa kulia Cholo alikuwa anamuweka hatarini kwa kuruhusu hatari nyingi zipite upande wake na hata goli lilipitia huko . Kwa muda mrefu hakuwa mchezoni kwa kuwa mpira ulikuwa ukibutuliwa hovyo na kila timu na pia walinzi wake wa kati walikuwa makini sana kuondoa hatari nyingi langoni mwake . (7/10)
2.Nassoro Cholo.
Kwa mchezo wa jana unaweza kusema kuwa mojawapo ya watu ambao waliigharimu Simba alikuwa cholo , alikuwa akijitahidi kuwakabili viungo wa Simba lakini hakuwa akifanya hivyo kwa kutumia maarifa na mara nyingi alikuwa akisababisha faulo ambazo zilikuwa zilikuwa zinahatarisha lango la Juma Kaseja na pia hakuwa akipandisha mashambulizi kusaidiana na na kiungo aliyekuwa akicheza upande wake . (4/10 )
3.Amir Maftah .
Alicheza katiaka kiwango cha kawaida ambacho huwezi kusema kuwa ni cha juu ama cha chini , kuna wakati alitimiza majukumu ya nafasi yake na kuna wakati alikuwa akipoteza umakini japo alijitahidi vilivyo kuwamudu Godfrey Taita na Jullius Mrope na hawakuleta madhara upande wake labda uchezaji wa Taita ndio ulimfanya awe na wakati mzuri mchezoni . (5/10)
4.Juma Said Nyoso.
Nyoso kama kawaida yake alikuwa moja ya watu ambao walihakikisha lango la kaseja halidhuriki , alikuwa akiwakabili washambuliaji na viungo wa Yanga kwa ujasiri mkubwa na mchezo wake wa kutokuwa na masihara awapo kazini ulimpa alama nyingi mchezoni ,alikuwa aki-link vizuri na mwenzie Yondani . ( 7/10)
5. Kevin Yondani
Kama ilivyokuwa kwa nyoso Yondani hakucheza vibaya , alikuwa makini kwenye eneo lake ambalo mara nyingi halikudhurika na na movement za washambuliaji wa Yanga , dosari pekee kwenye mchezo wake zilikuwa pale ambapo alikuwa anakubali kuvutika kirahisi kwa ujanja aliokuwa anautumia Jerry Tegete wa kumuondoa kwenye eneo lake na kutengeneza mwanya ambao kama washambuliaji wa Yanga wangekuwa makini wangeweza kuwafunga Simba ila alicheza vizuri kwa ujumla japo mchezo wake uliingia dosari pale alipoteleza na kumpa mshambuliaji wa Yanga Keneth Asamoah mwanya muhimu wa kufunga bao lililoipa Yanga ubingwa . ( 6/10)
6.Mwinyi Kazimoto.
Kitu kilichoamua mchezo kwa upande wa Simba ilikuwa ni kuumia kwa Mwinyi Kazimoto ambaye aliipa uhai miubwa sana safu ya kiungo ya Simba , alikuwa na hamu na mpira na alikuwa akiufanya kama anavyotaka , alikuwa aki-penetrate kwenye ngome ya Yanga kwa kujiamini kwa hali ya juu na kutoka kwake kulirejesha pumzi kwenye safu ya kiungo ya Yanga , kwa dakika chache alizocheza hakika alikuwa nyota kwa upande wa Simba .( 8/10 )
7.Shija Mkina .
Kwa dakika alizocheza alikuwa moja ya watu waliokuwa na uhai kwa Simba , kwenye kipindi cha kwanza alitengeneza nafasi mbili za uhakika ambazo kama zingefanyiwa kazi kwa umakini basi matokeo yasingekuwa yale yalioamua mchezo , alikuwa akipanda na kushuka kwa nidhamu ya hali ya juu ambayo itamshawishi kocha yoyote kumpa nafasi kwenye kikosi chake japo kuna wakati ukosefu wa uzoefu wa mechi kubwa ulionekana kumuathiri kwa jinsi alivyokuwa akifanya maamuzi yake akiwa na mpira mguuni, kwa bahati mbaya mechi ilimzidi nyakati za mwisho za mchezo na alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Salum Machaku. (7/10 )
8.Patrick Mutesa Mafisango.
Ukimuacha Mwinyi , Shija na Ulimboka mchezaji mwingine aliyeipa Simba uhai ni huyu jamaa toka Rwanda , Mafisango ana akili nyingi sana ambazo hatuzioni kwa wachezaji wetu , anapopata mpira haupotei na pasi zake ni za umeme na si za mkaa , ni mfano halisi wa kiungo anavyotakiwa kucheza , kilichofanya mchezo wake usiwe na madhara kwa Simba ni wenzie kushindwa kuelewa aina ya Soka ambalo Mafisango analicheza kwani kama ingekuwepo “chemistry” kati yake na wenzie basi Simba ingefaidika sana na uwepo wa Mafisango. ( 7/10 )
9.Musa Hassan Mgosi .
Kwa nafasi aliyocheza Mgosi hakuwa na la kufanya zaidi ya yale aliyoyafanya kwa sababu hakulishwa ipasavyo japo kuna nyakati ambazo angeweza kufanya juhudi zaidi na kuipa msaada timu yake na hakufanya hivyo , kinachomgharimu Mgosi ni ukweli kwamba si mshambuliaji wa kuzaliwa , huyu ni kiungo-winga anayelazimika kucheza nafasi ya ushambuliaji na ndio maana huwa anakumbana na lawama za kupoteza nafsi nyingi sana . ( 6/10 )
10.Haruna Moshi Boban .
Haruna ni moja kati ya wachezaji wachache wa ukweli ambao Tanzania inaweza kujivunia kuwa nao , ana vitu vingi vya ziada ambavyo wenzie wengi wanavikosa , alikuwa akitengeneza nafasi nyingi sana kwa Simba lakini shida kubwa waliyo nayo Simba ni kumkosa mtu ambaye anaweza kuzifanyia kazi pasi za kina Haruna na kina Mafisango. Tatizo kubwa la Haruna ambalo litaendelea kumhukumu kwenye soka la miaka ya sasa ni kutokuwa na ujasiri , Haruna ni mchezaji wa kwanza kukubali matokeo na kuweka silaha chini , hili lilionekana kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Al Mareikh na hata kwenye fainali dhidi ya Yanga ambapo alionekana kuchoka mno na sura yake ilikuwa inaonyesha kuwa alikuwa anaomba mchezo uishe haraka ili ajiondolee balaa .( 6/10)
11.Ulimboka Mwakingwe.
Ulimboka alicheza vizuri sana kiujumla, hakuna makosa mengi ambayo aliyafanya ana alidhihirisha ukongwe wake ambapo uzoefu alio nao wa mechi kubwa kama hii ulimsaidia, alikuwa mtulivu na hakuwa na papara nyingi , alijitolea mno kwa timu yake akipanda na kushuka na wakati mwingine “ku-switch flanks” na Shija Mkina jambo ambalo liliwachanganya walinzi wa Yanga , kwa upande wa Simba Uli ni moja ya watu waliocheza vizuri ingawa alikosa bao la wazi kipindi cha kwanza. Lakini pia mpira alioupoteza ndiyo uliozaa bao la Yanga (6/10)
Walioingia.
Mohamed Banka .
Hakika kama ambavyo Nurdin Bakari alichukua sifa ya “man-of-the –match” basi Banka anastahili ile ya “flop-of-the-match”, Banka aliigharimu Simba sana kwa aina yake ya uchezaji ambapo alikuwa mzito sana wa kufanya maamuzi ,alipenda kufanya “dribbling” ambazo hazina maana yoyote , hakuna pasi yoyote inayoongea ambayo aliipiga na mchezo wa Simba uliamuliwa na kuingia kwake ambapo mchezaji aliyekuja kuchukua nafasi ambaye alitoka baada ya kuumia alifanya mengi mno ambayo Banka alikuja kuyaua kabisa . (4/10 )
Salum Machaku.
Salum nbi cmhezaji ambaye bado hajakomaa kuichezea klabu kama Simba , bado jezi nyekundu na nyeupe ni nzito sana mwilini mwake na hatambui majukumu anayokuwa nayo mchezaji wa Simba awapo uwanjani hasa anapokuwa uwanjani kwenye mchezo dhidi ya Yanga , ana mchezo wa kitotona wa kizamani ambao hakika si Tanzania tu hata ulaya hauna tena nafasi , anakaa na mpira bila kuwa na malengo nao, na zaidi ya yote hajawa tayari kubadili mtindo wake wa uchezaji , jana angeweza kuwa mtu muhimu sana kwa Simba kwa upande wake kwa kuwa ni mtu mwenye kipaji na mwenye uwezo mkubwa ila hatumii maarifa kusaidia kipaji chake , ni dhahiri kocha Moses Basena alikuwa na malengo na kumuweka benchi akilenga kumtumia kama Super-sub pale ambapo mpinzani anapokuwa amechona kwa jinsi alivyo na uwezo wa kumiliki mipira , kupiga chenga, kasi na uwezo wake wa kupiga krosi hatari lakini alimuangusha kocha sana kwa kuwa alipoingia alionekana kama yeye ndio alikuwa amechoka na Nsajigwa alikuwa ameingia kwa kuwa alikuwa anamkabili na kummudu kwa urahisi sana . ( 3/10 )
Salum kanoni .
Salum Kanoni aliingia huku kocha akiwa na mawazo ya penati kwa sababu kanoni ni moja kati ya wapiga penati wazuri ambao simba inao ila haikuwa hivyo kwa kuwa aliingia na Simba ikafungwa hivyo alihitajika kuiokoa timu yake , hakuwa makini kwa yale aliyokuwa akiyafanya , alipata nafasi mbili za kupiga mashuti lakini hakuwa makini na aliishia kupaisha jukwaani . (-)
Kocha Moses Basena.
Mpaka sasa bado ni mapema nab ado anahitaji muda wa kuingiza falsafa yake kwenye timu japo bado anaonekana kuwa si mkali kwa wachezaji wake ambao hawana umakini na bado hawana ari ya upiganajni ambayo iko kwa wenzao Yanga , bado hatujaona mkono wake kwenye usajili ila anahukumiwa kwa usajili wa Derick Waluhya ambaye anaonekana kusajiliwa kwa kukurupuka mno .
Shaffih kwa analysis yako yako uliyotoa imekaa kinazi kuliko kiuanamichezo. Kwa pwenti ulizowapa wachezaji wa Simba na pwenti ulizowapa wachezaji wa Yanga hazilingani na matokeo ya mchezo huo! Kwa hizo 'pwenti' finyu ulizowapa Simba, nini kilwazuia Yanga wasiibuke na mvua ya magoli? Au unaataka kuniambia dhamira ya Yanga ilikuwa ni kushinda goli moja kwenye muda wa dakika 120? Jamani tuache ushabiki na hasa tunapokuwa na dhamna kubwa kama tulizonazo. Shaffih kama hujui una dhamana kubwa sana ya kuwahabarisha wanamichezo hapa kwenye Blog yako na kule Clouds na hata njiani ukutanapo na watu. Punguza ushabiki. Yanga wameshinda kimatokeo lakini kimpira Yanga walizidiwa. Kilichowagharimu Simba ni kukosa mtu wa mbele vinginevyo usingekuwa unaandika haya unayoyaandika kwa kukidhi matarajio yako. Kaka mimi ni mfuasi wako sana lakini naanza kuingiwa na mashaka. Maestro ni kiongozi kabisa wa Simba, Mayai ni Kiongozi wa Yanga, ninapowasikiliza kwenye Sports Round Up naona kabisa they dont want to be influenced by their club positions. Lakini wewe kaka TOO MUCH! Acha washabiki walonge wanavyotaka. Wewe eleza ukweli.
ReplyDeleteMkelemi (mkelemi@facebook.com)
Mbeya