Search This Blog

Sunday, July 24, 2011

Historia ya upinzani baina ya miamba ya soka nchini Kenya AFC Leopards na Gor Mahia .

Mchezo wa soka duniani kote unaongezwa ladha na upinzani . Mahali kokote utakapokwenda hata uswahilini ambako kuna soka la mpira wa makaratasi lazima utakuta kuna timu mbili ambazo zina upinzani mkali ambao ndio hasa unanogesha mechi baina ya timu hizo.Hapa nchini kwetu kuna Simba na Yanga , Afrika Kusini kuna Orlando Pirates na Kaizer Chiefs ,nchini Misri kuna National Al Ahly na Zamalek,nchini Ghana kuna Asante Kotoko na Hearts of oak , Argentina kuna Boca Juniors na River Plate , Italia kuna AC na Inter Milan,Serbia Kuna Red Star na Partizan Belgrade ,na nchini Kenya kuna AFC Leopards na Gor Mahia .
AFC Leopards na Gor Mahia ni timu ambazo zina upinzani wa kifo na uhai. Timu hizi ziliundwa kama timu za makabila miaka ya sitini ambapo AFC Leopards walikuwa wakiwakilisha kabila la Abaluhya na Gor Mahia wakiwakilisha kabila la wajaluo na tangu kuundwa kwake zimeliteka soka la Kenya na katika wakati Fulani soka la Afrika .Timu hizi zilitoka kuwa klabu za makabila na upinzani wake umefikia kuwa upinzani uliotapakaa nchi nzima kiasi kwamba kila timu hizi zinapokutana zinaunda kitu kinachoitwa The Great Kenyan Derby tofauti na hapo awali ambapo mechi hii iliitwa The Western Derby kutokana na eneo la kijiografia ambako timu hizi zilipoanzishwa ambako ni mashariki mwa nchi ya Kenya .


Tangu vilabu hivi vilipoanzishwa hadi leo hii vimeweza kuchangia zaidi ya asilimia 90% ya wanasoka bora nchini Kenya ambapo wengi wao kabla ya kwenda kwingine walianzia kwenye eidha jezi za kijani ambazo ni za Gor Mahia au za michirizi myeupe na bluu ya AFC Leopards au kwa wengine wakicheza pande zote mbili kama vile James Siang’a , Wiolliam Chege Ouma na Dan Shikanda .
Katika miaka iliyopita ambapo timu hizi mbili zilikuwa miamba ya soka nchini Kenya mechi baina ya wapinzani hawa ilikuwa ikiamua ubingwa wa soka nchini Kenya .Kama Mojawapo ingeshinda mara mbili au mara moja na kutoka sare mchezo unaofuata basi ingetangaza ubingwa na hii ni kwa sababu timu hizi zilikuwa ndio hasa zenye uwezo wa kisoka na kifedha kuliko timu zingine kama ilivyo hapa Tanzania kwa Simba na Yanga au Hispania kwa Mdrid na Barca . Kama Gor Wangetwaa ubingwa mwaka huu basi AFC wangetwaa mwakani na huo ndio ulikuwa utaratibu miaka hiyo .
Zinapokutana timu hizi mbili mbinu zote za ushindi hutumika , ndani na nje ya uwanja hupiganwa vita kali ambayo inachagizwa zaidi na ukweli kwamba kila wanapokutana wapinzani hawa ni zaidi ya soka , ni zaidi ya matokeo ya uwanjani kwani watani hawa wajaluo na waluhya wameanzia upinzani wao kwenye kabila na soka ni moja ya maeneo ambayo utani wao unaamuliwa ambapo anajulikana mbabe na mnyonge .Msimu uliopita watu kadhaa walipoteza maisha baada ya kutokea mkanyagano kwenye uwanja wa Nyayo ambako vilabu hivi vilikuwa vikimenyana na hiyo itakuonyesha jinsi mechi baina ya watani hawa inavyowavutia watu nchini nzima .


Pamoja na ukweli kuwa timu hizi ni za wajaluo na waluhya ukweli ni kwamba upinzani hauko tu Mikoa ya nyanza kwa wajaluo na Western au magharibi kwa waluhya bali toka Mombasa hadi Machakos , Nairobi na Nakuru utakuta mashabiki wa Gor Mahia au AFC Leopards . Zamani mchezaji wa kiluhya ambaye angediriki kucheza Gor Mahia angejikuta akitengwa na jamii nzima ya wanakabila wenzie na si ajabu ukikuta mtu huyu akiwa mpweke akiugua au akiuguliwa na hata akifiwa au kwenye sherehe za kimila kwani anahesabika kama msaliti asiye na aibu na vivyop hivyo kwa Mjaluo ambaye angejaribu kuvaa jezi za bluu na nyeupe za AFC .
Afc Leopards ilizaliwa rasmi mwaka 1942 baada ya klabu za daraja la kwanza za watu toka kabila la luhya za Marama , Samia United na Bunyore zilipoamua kuungana na kuunda timu moja .
Moja ya wachezaji maarufu waliowahi kuvaa nyuzi za AFC ni kama Joe Kadenge ambaye ni sawa na Pele kwa Kenya , Jonathan Niva , Joe ‘jj’ Masiga , Wilberforce Mulamba , Mike Amwayi , Mickey Weche, Murila , Nyawanga , Aggrey Lukoye na Peter Lichungu na wengine kama Francis Oduor na nahodha gwiji wa Harambee Stars Musa Otieno.
Kwa upande wa Pili Gor Mahia yenyewe ilianzishwa miaka mine baada ya wapinzani wake AFC mwaka 1968 na kama wenzao kuzaliwa kwake kulikuja baada ya muungano wa timu mbili za watu wa kabila la Luo (wajaluo) Luo Union na Luo Stars . Gor kwa upande wao wametoa mchango mkubwa katika nyota waliowahi kulipaisha jina la Kenya kwenye ramani ya soka . Baadhi ya watu hao ni kama vile Allan Thigo, Sammy Owino Kempes , John Bobby Ogola, Nashio Oluoch Lule, Austin Oduor , David Ochieng Kamoga,John Okelo Zangi, Peter Otieno Bassanga, Ben ‘breakdance’ Oloo, Tobias Ocholla na Sammy Onyango Jogoo pamoja kocha wa sasa Zedekiah Otieno ‘zico’ ambaye ndiye nahodha wa mwisho wa Gor Mahia kubeba ubingwa wa ligi ya Kenya mwaka 1995.
Tangu miaka ya 70mpaka ya 80 Gor na AFC ndio vilbeba soka la Kenya vikibadilishana mataji ya ubingwa wa ligi ya Kenya kama mbio za vijiti huku wakihamishia upinzani huo kwenye ubingwa wa CECAFA japo katika mwaka wa 1987 Gor Mahia waliwazidi wenzao kete kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika katika kombe la Mandela .
Klabu hizi zilipata wakati mgumu kwenye miaka ya tisni ambapo hali ya ugumu wa uchumi iliyoikumba nchi ya Kenya ilishuhudia vilabu hivi vikikumbwa na ukata ambao ulimaliza utawala wao kwenye soka nchini Kenya .Sambamba na ukata vilabu hivi vilimalizwa na upinzani wa kisiasa ambao ulikuwa mkali nchini Kenya huku vilabu hivi vikitumiwa na wapinzani kukiua chama tawala cha KANU .
Huku vilabu hivi vikiwa sawa katika historian a vitu vingine vingi kama vile mapacha kwa pamoja vilijikuta vikishuka daraja kwenye ligi ya Kenya katika vipindi vya miaka 2004 na 2009.
AFC walishuka daraja mwaka 2006 na walicheza ligi daraja la kwanza mwaka 2007 na mwaka 2008 na waliweza kupanda msimu uliofuata .

Timu hizi zinakutana kwenye ligi ya soka nchini Kenya siku ya Jumapili tarehe 24 huku Gor mahia wakiwa na nguvu kulinganisha na wapinzani wao baada ya kuwa na msimu mzuri ambapo walimaliza ligi nyuma ya mabngwa Ulinzi Stars . Gor wanaonekana kuwa vizuri na nje uwanja pia ambapo chini ya uenyekiti wa Ambrose Rachier ambapo msimu huu wameweza kupata mkataba wa udhamini wa jezi zao kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu yao .
AFC Leopards wamekuwa na homa za vipindi huku wakihangaika sana kutafuta gia tangu waliporejea kwenye ligi kuu. Mabadiliko ya kia mara kwenye uongozi yamechangia sana kuiumiza klabu hii ya waluhya . Katika kipindi cha miaka miwili AFC Leopards wamebadilki makocha mara zisizopungua 9 na wenyekiti mara mbili na kwenye mazingira kama haya hakika mafanikio yanakuwa magumu kupatikana .
Pamoja na tofauti hiyo kwenye mafanikio , siku zote vilabu hivi ndio vionalitengeneza soka la Kenya kwa miaka yote na ukitaka kuhakikisha hilo tazama rekodi ya mataji ya ligi kuu ya Kenya na utaona hilo , timu hizi zimetwaa ligi ya Kenya mara 12 kila moja na siku zote zinapokutana kila mmoja antamba kuwa yuko juu ya mwenzie , je hiyo tarehe 24 ni Gor mahia mabao wamekuwa na nyumba tulivu hivi karibuni ambao wataweza kuwapa raha wajaluo au AFC Leopards ambao wamekuwa wakitibuana kila leo ambao wataanza maisha mapya ya mafanikio kwa kuwachapa wapinzani wao , dakika tisini ndio zaitakazoamua.

No comments:

Post a Comment