Hatimaye matarajio ya watanzania wengi yametimia kwani michuano ya Kagame Castle Cup inafikia tamati kwa mchezo wa fainali unaowakutanisha wenyeji Simba na Yanga . Kama ungemuuliza shabiki yoyote wa vilabu hivi nani angetwaa uchampioni wa michuano hii mwanzoni ni dhahiri angekwambia kuwa timu yake itashinda hivyo njia pekee ya kumaliza ubishi huu ilikuwa kukutana kwenye mchezo wa fainali anayeshinda ashinde na anayefungwa angoje siku nyingine .
Ukitazama timu hizi mbili kila moja ina sehemu yake ambayo inaipa kiburi na uhakika wa kuibuka ushindi lakini upande wa pili nao kila timu ina mapungufu yake ambayo yanaipa woga .
Besena na Falsafa ya ulinzi..
Makocha wa timu hizi mbili kidogo wamekuja na falsafa tofauti hasa kwa kocha wa Simba Moses Basena . Mganda huyu ameifanya Simba iwe na safu ya ulinzi ambayo ina uimara ambao ulikosekana msimu uliopita wa ligi ya Vodacom . Labda hii ni kwa sababu timu hii imekosa wamaliziaji huku ikiwa na viungo wengi ambao wanapenda kuuchezea mpira hali inayoweza kuwagharimu wanapokutana na timu inayolinda kwa nidhamu ya hali ya juu na ndio maana hadi michuano hii inafikia hatua ya fainali Simba imeruhusu wavu wake kuguswa mara mbili tu . Hivyo nadhani ni sahihi kusema kuwa Basena ana falsafa ambayo inazingatia zaidi ulinzi.
Sam Timbe Kuimalisha kiungo…
Kwa upande wa Jangwani mganda mwingine Sam Timbe anaonekana kuwa mtu ambaye anapenda timu yake ishambulie mwanzo mwisho huku ikiwatumia walinzi wanaotumia nguvu sana wakati wanapokabiliana na washambuliaji toka timu pinzani , labda ni kwa sababu ya aina ya uchezaji wa walinzi alio nao ambao ni watu “physical” kina Fusso,Cannavaro,Taita na Oscar Joshua. Timbe anaonekana kuwa ameibadilisha Yanga kwa kiasi kikubwa kwenye safu ya kiungo ambayo inaongozwa na Rashidi Gumbo mchezaji aliyesajiliwa toka Simba akishirikiana na kiungo mwingine Nurdin Bakari ambaye naye alitoka Simba muda mrefu kidogo uliopita .Watu hawa wameonekana sana kuelewana kwenye safu ya kiungo tofauti na ilivyo falsafa halisi ya Yanga ambayo kihistoria hupenda kuwatumia zaidi mawinga kama kina Ngassa, Nsa Job , Edibily Lunyamila na wengine wengi waliopita siku za nyuma japo hawajaitupilia mbali falsafa hii kwani wapo Julius Mrope na Kiggi Makasi . Safu ya Ushambuliaji ya Yanga ndio inayoonekana kuwa na uhai zaidi unapopambanua safu mbili za ushambuliaji za Simba na Yanga . Hadi kufikia fainali Yanga imetupia wavunia mabao saba kwenye hatua ya makundi na kwenye mechi za mtoano walishindwa kufunga bao hata moja na kupita kwa njia ya matuta. Simba wao wamefunga mabao sita hadi kufikia hatua hii.
Simba kutokua na mshambuliaji asilia…
Ukitazama vikosi vya timu zote mbili Yanga wanaonekana kuwa kamili kuliko Simba kwani wanaonekana kuwa na “first eleven” inayoeleweka na ambayo inaweza kujenga “chemistry” yaani maelewano tofauti na Simba ambao kikosi chao sio kile kile na kimekuwa kikibadilika badilika sana karibu kila mechi . Unaweza kukuta leo Banka anacheza nafasi ya namba tisa , kesho akacheza kumi na mwenendo ndio umekuwa huo karibu kila mechi .
Hili linaweza kuwa na hasara au faida kwa sababu wakati mwingine mpinzani anaweza kukosa mbinu ya kukabili kwa sababu tu ameshindwa kujua ni timu ipi itakayoingia siku hiyo na hasara yake ni pale ambapo timu yako haina “chemistry” kitu ambacho Yanga wanaonekana kuwa nacho .Simba tangu mchezo wa kwanza dhidi ya Vital O wamegharimiwa na tatizo moja kubwa ambalo ni kukosa wamaliziaji , hili limesababisha wekundu kukosa mabao mengi sana ya wazi . Ukitazama mfumo ambao wanaingia nao ambao huwa unabadilika badilika hata mchezoni Simba wamekuwa wakiwatumia mabeki wane , viungo wanne na washambuliaji (viungo wanaolazimika kucheza kama washambuliaji) wawili wanaocheza mmoja mbele mmoja nyuma katika mfumo wa 4-4-1-1 na wakati mwingine wanacheza 4-4-2 diamond huku kiungo mmoja akisimama mbela ya mabeki na mwingine nyuma ya washambuliaji na hata wakati mwingine wamekuwa wakicheza 4-1-3-2 au 4-1-3-1-1 ambapo mara nyingi unakuta kaseja anasimama langoni chollo akisimama kulia , amir maftah akisimama kushoto na wawili kati ya Waluhya Derick,Kevin Yondani na Juma Nyoso wakisimama kati na kuna wakati Derick waluhya alisimama pembeni kulia jambo ambalo almanusra liwaletee Simba balaa na kwenye safu ya kiungo Jerry Santo amekuwa akisimama kama namba sita kwenye nafasi ya holding au combat midfielder akiwa mchezaji pekee kwenye safu hiyo aliyecheza kwa “consistency” ya hali ya juu huku pembeni kulia akicheza wakati mwingine Salum Machaku na wakati mwingine Ulimboka na Musa Hassan Mgosi amekuwa akicheza kama kiungo anayetokea upande wa kushoto na Shija Mkina amekuwa akiingia tokea benchi la wachezaji wa akiba kujaza nafasi ya winga ya kulia . Safu ya viungo wa Simba imejaa watu ambao wanajua kuuchezaea mpira kwa ufundi wa hali ya juu na wanapiga pasi nyingi sana nzuri ila shida kubwa imekuwa kwenye umaliziaji ambako Mohamed Banka na Haruna Moshi wamekuwa wakipangwa kama washambuliaji. Watu hawa wawili kiasili ni viungo ambao wanacheza namba nane au kama wakicheza ushambuliaji wanacheza namba kumi nyuma ya mshambuliaji .Sasa wanapocheza kama washambuliaji Simba inakosa mabao mengi sana kwa kuwa hawa watu si wafungaji ufundi wao wote unaishia kwenye pasi za mwisho na sio kuzipasia nyavu .
Mfumo wa Yanga ni 4:4:2 na 4:4:1:1
Kwa upande wa Yanga wamekuwa wakitumia mfumo wa 4-4-2 au 4-4-1-1 yaani mabeki wakiwa kwenye mstari mmoja , viungo kwenye mstari mmoja na washambuliaji wawili moja nyuma ya mwingine . Godfrey Taita,Shadrack Nsajigwa , Oscar Joshua , Chacha Marwa na Nadir Haroub Canavaro wamekuwa wakisimama kwenye mstari wa walinzi wa Yanga na kati ya hawa Chacha Marwa ameonekana kuwa “outstanding ” kuliko wenzie kwa jinsi anavyocheza kwa ujasiri akikabiliana na washambuliaji kwenye zile “one-to-one situation” . Kwa walinzi wa Yanga shida imekuwa moja nayo ni kutumia nguvu nyingi kuliko maarifa na wakati mwingine wanapokutana na washambuliaji wanaocheza ‘begani’ mwa beki wamekuwa wakichanganyikiwa kama ilivyotokea kwa Jonas Sakuwaha wa AL Mareikh na Owen Kasule wa Bunamwaya ambapo mara zote hizo Yanga walijikuta wakiruhusu mabao ya kizembe . Viungo wa yanga wamekuwa wakicheza vyema , Nurdin Bakari amekuwa aki-link vyema na Rashid Gumbo na Julius Mrope kwa upande wake amekuwa akiwapa wakati mgumu sana mabeki kwa kasi yake na chenga , Kiggi Makasi yeye ameonekana kuwa na homa za vipindi kwani kuna wakati anakuwa hayuko mcchezoni ana anakuwa anaipa timu yake wakati mgumu kwani inakuwa kama inacheza pungufu japo mipira yake anayoileta toka upande wa kushoto ina madhara sana .
Washambuliaji wa Yanga ndio wamekuwa gumzo haswa Hamis Kiiza na Davis Mwape japo jinsi wanavyotumiwa kidogo inatia mashaka . Davis Mwape amekuwa akilazimika kucheza nyuma ya mshambuliaji mwingine jambo ambalo kwa mwili wake mkubwa linamshinda kwa sababu anashindwa kupima dribbling zake , kuna wakati ambapo anashindwa kupiga mahesabu ya wakati gani wa kuusogeza mpira na wakati gani wa kuupiga , kama angekuwa kiungo hili lisingempa shida ila kwa kuwa yeye ni aina ya wachezaji tunaowaita “18 yard players” yaani mchezaji wa kwenye eneo la 18 tu na nje ya hapo si mahala kwake . Pamoja na hayo ameweza kufunga mabao mawili ambapo mojawapo alilofunga dhidi ya Bunamwaya lilikuwa bao muhimu kwani liipa Yanga ushindi ambao uliwahakikishia uongozi wa kundi . Hamis Kiiza kwa upande wake ameonyesha umahiri wake kwenye ufungaji na kama Simba hawatampa ulinzi wa kutosha hakika atawaliza .
Kukosekana kwa Boban na Santo
Tatizo moja ambalo Simba watakuwa nalo kwenye mchezo wa fainali dhidi ya watani wao ni kuwakosa Haruna Moshi na Jerry Santo ambao wana kadi mbili zilizofuatana . Wote walipata kadi za njano kwenye mechi ya Robo fainali dhidi ya Bunamwaya na wakapata teka kadi kama hiyo dhidi ya Al Mareikh kwenye nusu . Kati ya hawa Simba watamkosa sana Jerry Santo mtu ambaye ukimuacha Juma Kaseja kama Simba wakitwaa ubingwa huu basi anaweza kuwa mchezaji wao wa michuano . Santo ni mtu anayetambua majukumu yake na anayatimiza kwa asilimia zote . Kukosekana kwa Boban kunaweza kusiwe pengo kubwa kwa sababu wapo watu ambao wanaweza kujaza nafasi yake vyema . Kumkosa Santo kunaweza kumaanisha kuwa Basena akalazimika kumtumia mtu kama Waluhya kama jeraha lake litapona katika nafasi ya kiungo wa chini au Patrick Mafisango japo Mafisango ni mzuri sana kwa kiungo cha juu .Kwa upande wa Kevin Yondani na Juma Nyoso watakuwepo japo Derick Waluhya kama atapona atakuwa na umuhimu wake kwa jinsi alivyo na uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo kuwaliko wenzie anaopigania nao nafasi ya beki wa kati, Ulimboka mwakingwe ameonyesha kiwangi kizuri katika mechi zake zote alizocheza na uzoefu wake wa mechi kama hii unampa faida ya ziada ya kupewa nafasi . Kama kanuni ziotaruhusu na kama Simba walisajili mapema jina la Mwinyi kazimoto na kama atapangwa atakuwa na umuhimu kwa jinsi anavyojua jukumu la “playmaker” na anaweza kuwa na mchango mkubwa sana.
Yanga na kikosi kamili..
Yanga wanaingia wakiwa na kikosi kizima ambacho hakina mapungufu yoyote . Golini akiwepo Yaw Berko ambaye ukiacha kungushwa na mabeki wake ni “reliable” sana golini , Nsajigwa , Taita , Canavarro na Chacha Marwa ni watu ambao wameonyesha uwezo wakiwa kwenye nafasi ya Ulinzi na hakuna sababu ya kutowapanga kwenye fainali , Gumbo na Nurdin moja kwa moja wana nafasi zao kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyo kwa maforward wawili Mwape na Kiiza japo rekodi inaweza kumfanya Timbe alazimike kumtumia Jerryson Tegete kwani amekuwa akiwafunga Simba mara kwa mara na uwepo wake uwanjani unawafanya walinzi wa Simba na kipa wao kuwa roho juu.
Sam Timbe vs Moses Basena..
Makocha wa timu zote mbili wana historian a Michuano hii . Sam Timbe amewahi kutwaa ubingwa mara tatu akiwa na timu tatu tofauti . Labda historia itampendelea tena na kumpa ubingwa wan ne na wa kihistoria . Bassena amewahi kucheza fainali mara moja ambapo alipoteza kwa Tusker Fc iliyokuwa inaongozwa na nahodha Jerry Santo katika mwaka ambao Yanga ilimkimbia mnyama kwenye mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu . je ataendelea na historia yake ya kuwasindikiza wenzie ?
Ukitazama historia ya vilabu hivi viwili kwenye michuano hii unapata sababu ya ziada ya kununua tiketi mapema na kuwahi kuingia uwanjani . Timu hizi zimewahi kukutana mara mbili ambapo kila mmoja ameshinda mara moja na atakeyeshinda safari hii atakuwa mbele ya mwenzie .
Itakuwa fainali ngumu sana kwa sababu timu hizi zina historia ambayo iko mbali zaidi ya michuano hii na kwa kila mmoja kumfunga mwenzie kwa njia yoyote ile ni jambo la thamani kubwa sana na mchezo huu unaongezewa utamu na ukweli kuwa ni mchezo wa fainali ambao lazima mshindi apatikane. Je itakuwa kijani na njano au nyekundu na nyeupe ambao wataitawala Afrika mashariki na kati? Jibu litapatikana baada ya dakika tisini au 120 au baada ya mikwaju ya penati iwe mitano au ile ya piga ni kupige hadi mtu afe .
prediction:Mshindi atapatiana baada ya dakika 90.
No comments:
Post a Comment