Search This Blog

Sunday, July 31, 2011

Chimbuko la utawala wa wahindi katika soka la Tanzania

UKIANZA kuelezea historia ya soka Tanzania, bila shaka utaelezea miaka ya kuanzia 1970 kwenda mbele na si kurudi nyuma kutokana na uhalisia.

Nchi yoyote duniani lazima iwe na mfumo wake wa soka ili kutimiza malengo yake katika mpira wa miguu. Unaweza kuona jinsi Afrika Magharibi ilivyo na shule nyingi za soka.

Hapa chini, kuna maelezo kidogo yanayoeleza jinsi Tanzania ilivyoweza kutoa wachezaji wake katika miaka ya nyuma.

Mwaka 1970- 1976
Kwa Tanzania wakati wa miaka ya 1970, wachezaji waliojiunga na klabu zilizokuwa zikishiriki ligi walikuwa wakipatikana kwa njia ya kuibua vipaji kutoka mitaani na katika timu zilizokuwa zikishiriki michuano ya katika vijiji na majiji.

Wachezaji kama Adam Sabu, Kitwana Manara, Abdallah Kibaden, Jumanne Hassan ‘Masimenti’, Gibson Sembuli waliweza kufanya vizuri na kuweza kuwa kwenye chati kwa muda mrefu.

Chimbuko lao kiuchezaji, ndilo lililopelekea waweze kucheza kwa muda mrefu tofauti na sasa, mpango huu unaelezwa kwamba uliweza kutoa wachezaji wengi wenye vipaji na moyo wa kucheza soka kuliko sasa.

Ndani ya kipindi hiki, jamii iliendelea kumiliki timu na kuwekeana upinzani kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa.

Mwaka 1976-1982
Hiki ni kipindi ambacho wachezaji wengi walikuwa wakitokea shuleni na vyuoni na kipindi kinachoelezwa kuwa kilitoa wachezaji wengi waliokuwa wanaona mbali katika soka na maisha.

Wachezaji kama Mohamed Salim, Thuwen Ally, Peter Tino, Omar Hussein, Adolph Richard, Leodegar Tenga, Mtemi Ramadhan, George Kulagwa waliweza kung’ara lakini miongoni mwao wako waliokuwa wakitumikia vitu viwili; shule na soka.

Watu kama Tenga, Mtemi na Laurence Mwalusako wanaweza kuwa mfano wa jambo hili hadi leo hii.

Ni kipindi hiki ambacho wachezaji wake waliweza kucheza kwa moyo wote na kufanikisha ushiriki wa Tanzania katika michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980.

Ndani ya kipindi hiki timu za makampuni zilianza kuchomoza, lakini bado zilitegemea wachezaji kutoka shuleni na vyuoni ili kujiimarisha.

Mwaka 1982-1988
Ingawaje timu za makampuni na mashirika ya umma zilianza kushamiri tangu mwaka 1975, lakini kipindi hiki kinaelezwa kuwa kilikuwa cha timu hizo kutamba.

Timu kama Pamba, CDA, Bandari, Bima, Tegry Plastics, Tumbaku Moro, RTC Kagera na nyinginezo ziliweza kung’ara na kutishia uhai wa timu nyingine kama Simba, Yanga, Coastal Union, African Sports na nyinginezo.

Hapa wachezaji walikuwa wakicheza soka kama ajira kwao, kwani waliajiriwa katika kampuni hizo kama ilivyo kwa waajiriwa wengine, lakini wao wakiwa na jukumu la kucheza soka pekee.

Mchezaji Rashid Idd anaweza kukumbukwa jinsi alivyoingia katika kikosi cha timu ya taifa mwaka 1978 akitokea katika michuano ya mashirika na makampuni ya umma (Shimuta).

Idd, aliweza kung’ara katika michuano hiyo ambayo wakati huo ilikuwa na taswira kubwa tofauti na sasa, kiasi cha Kocha wa timu ya taifa kuishuhudia ili kuweza kupata wa watakaofaa kwa timu yake.

Licha ya timu za mashirika ya umma kutamba, pia klabu nyingine ziliweza kuteka soka la Tanzania na kuzima utawala wa Simba na Yanga.

Pamoja na hali hiyo, bado timu za kijamii ziliweza kung’ara. Kwa mfano mwaka 1988 Coastal Union na African Sports za Tanga ziliweza kuwekeana ushindani mkubwa katika ligi na kupokezana kukalia kiti cha uongozi kwa muda mrefu.


1988 – hadi sasa
Baada ya hali ya timu za kijamii kama Simba na Yanga kuwa siyo nzuri wafanyabiashara walianza kujitokeza ili kuzifadhili.

Mohamed Virani ‘Babu’, anaweza kuwa miongoni mwa ‘wahindi’ wa kwanza kujitokeza kudhamini soka.

Hali ilizidi kushamiri mwaka 1990 pindi Abbas Gulamali(sasa marehemu), Azim Dewji na Shiraz Sheriff walipojitokeza moja kwa moja kuzifadhili Simba, Yanga na Pan African F.C ya Dar es Salaam.

Wakati Gulamali akiwa na Yanga, Dewji ambaye kwa sasa yupo na Moro United alikuwa akiisaidia Simba kuweza kurudi katika hali yake. Shiraz yeye alikuwa ndiyo mfadhili mkuu na meneja wa timu ya Pan African.

Wafadhili hawa waliweza kuwanunua wachezaji kutoka katika makampuni na mashirika ili kuimarisha timu zao.

Hussein Masha, Gerorge Masatu, wanaweza kuwa miongoni mwa wachezaji walioihama Pamba na kujiunga na Simba kutokana na ahadi za Dewji, pindi walipohama waliweza kuidhohofisha timu hiyo huku wakiipandisha chati Simba.

Hivyo hivyo kwa Yanga, ambao waliweza kumnyakua Edibily Lunyamila kutoka Biashara ya Shinyanga na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ kutoka Bandari Mtwara na kuimarisha kikosi chao.

Mafanikio ya Yanga na ufadhili wa Gulamali yaliweza kuonekana mwaka 1994 pale ilipotwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati huku Simba ikifanikiwa kufika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa na Stella Abidjan.

TIMU ZILIPO SASA;
Ukitoa timu za makampuni binafsi na taasisi za serikali kama Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Azam FC, African Lyon, Prisons, klabu nyingine za Ligi Kuu zilizobaki hazina chanzo cha uhakika cha fedha.

Nyingi zinaendelea kuwa imara kutokana na uhisani wa watu mbalimbali wenye mapenzi nazo, wengi wao hawana mikataba maalum ya kusaidia au kufadhili, jambo linalohatarisha uhai wake.

Moro United iliweza kutetereka baada ya kujiengua kwa waliokuwa viongozi wake, kama ilivyokuwa kwa Pallsons ya Arusha iliyokuwa chini ya uongozi Askofu Mollel.

No comments:

Post a Comment