ANDRE VILLAS BOAS-KOCHA MPYA WA CHELSEA
Hongereni sana Mashabiki wa Chelsea kwa kuajiriwa Andres Villa Boas kama kocha wenu mpya akija kurithi nafasi ya muitaliano Carlo Ancelotti .
Kwa kutazama rekodi ya Andres Villas Boas mashabiki wa Chelsea wana kila sababu ya kuwa na furaha kwa sababu kuu mbili . Nazo ni rekodi ya Villas Boas ambayo ameipata kwa haraka.
Andres Villas Boas ameweza kutwaa kombe La Ligi ya UEFA Europa , kombe la chama cha soka cha Ureno, pamoja na ligi kuu ya nchini Ureno.Hayo yote ameyafanya ndani ya misimu miwili tena akiwa na bajeti ndogo sana ambayo kwa kawaida haitoshi kusaidia timu kufanikiwa katika ulimwengu wa leo . Sababu kuu ya pili ni ukweli kuwa Andres Villas Boas ni mtu ambaye kiukweli anaujua mchezo wa soka na zaidi ya hilo anaifahamu vyema Chelsea kwani aliwahi kukaa kwenye benchi la ufundi la Chelsea chini ya Jose Mourinho hivyo ujio wake hautakuwa wa taabu sana na kuna uwezekano mkubwa kuwa anaweza asihitaji muda sana kuzoea mazingira ya Stamford Bridge pamoja na falsafa na mtindo wa timu ya Chelsea .
Tukitazama upande wa pili hapo ndio kuna utata zaidi . Labda turejee nyuma zaidi na kujiuliza kwanini aliyekuwa kocha wa Chelsea kabla ya ujio wa Villas Boas alifanya nini kibaya hadi kufukuzwa kazi . Carlo Ancelotti ni kocha aliyejijengea jina na heshima kubwa ulimwenguni kote . Heshima aliyonayo Ancelotti ni kutokana na kazi kubwa aliyoifanya akiwa na timu za Juvetus na AC Milan ambapo alitwaa mataji mengi ya ndani na nje ya nchi yake Italia . Kwenye msimu wake wa kwanza nchini England Carlo Ancelotti aliweza kulirejesha taji ambalo Chelsea ililipoteza kwa misimu mitatu taji la ligi kuu ya England , pamoja na hilo alifanikiwa kutwaa taji la kombe la FA.
Kitu ambacho Chelsea ya Roman Abramovich imeona kama kosa la jinai ambalo limemgharimu Ancelotti ajira yake ni kutotwaa taji la Ligi ya mabingwa barani Ulaya ambalo Roman Abramovich analitaka kwa udi na uvumba .Swali la kujiuliza ni moja , kwanini Chelsea imeukosa Ufalme wa ulaya ??? Kunaweza kukawa na majibu mengi kutoka kwa watu wenye mitazamo tofauti lakini nadhani jibu ambalo wote tutakubaliana nalo ni ukweli kwamba Chelsea walipokutana na Manchester United walizidiwa na timu ambayo ilikuwa bora zaidi yao.
Kusema kweli huwezi kujilaumu sana unapofungwa na timu kama Manchester United tena kwa mikwaju ya penalti , na zaidi ya hapo inapokuja ligi ya mabingwa kuna timu ambazo ubora wake huwezi kuufananisha wala kuupima . Mfano mzuri ni jinsi Manchester United walivyosasambuliwa na Barcelona kwenye fainali ya ligi hiyo ya mabingwa tena kwa mara ya pili wakirejea yale waliyoyashuhudia mwaka juzi mjini Rome . Kama Roman Abramovich angekuwa mmiliki wa United ina maana Sir Alex Fergusson angekuwa hana ajira ?
Kabla ya Ancelotti alikuwepo Avram Grant ambaye kama isingelikuwa mvua kubwa iliyonyesha na kumfanya John Terry ateleze na kukosa penati ya muhimu pengine angeendelea kuwa kocha kwani Chelsea walicheza vizuri usiku ule na bahati haikuwa yao kwani United walicheza vizuri mwanzo tu na baada ya hapo Chelsea walikamata usukani na kusawazisha bao la Cristiano Ronaldo mpaka mchezo kufikia hatua ya penati .
Bado kwa Abramovich suala la bahati mbaya halina nafasi na Grant aliondolewa na kazi yake akapewa Felipe Scolari ambaye hakukaa zaidi ya miezi sita , na kabla yake Chelsea waliwahi kuwa na mtu ambaye leo hii dunia nzima inamtambua kama kocha bora kabisa kwenye mchezo wa soka na rekodi yake ni ushahidi tosha juu ya ubora wake Jose Felix Mourinho . Alichokuwa anahitaji Mourinho ni muda na kuungwa mkono kwenye soka la wachezaji na sidhani kama Mourinho angepewa misimu mitano Chelsea angeshindwa kuwafanya wawe mabingwa wa Ulaya . Mbona alifanya hivyo ndani ya misimu miwili tu akiwa Inter ?
Maelezo hayo yote yanaonyesha kuwa tatizo lililopo Chelsea si kwa makocha bali ni mmiliki mwenyewe . Tangu kabla ya mourinho alikuwepo Claudio Ranieri na mpaka leo hii Chelsea imekuwa na makocha sita na katika hao wote zimetumika fedha kiasi cha paundi million 50 kuwaajiri na kuwafukuza tu, jiulize swali moja je fedha hizi angepewa kocha mmoja kununua wachezaji Chelsea ingekuwa wapi?
Tatizo kubwa ni Roman Abramovich , mmiliki asiye mvumilivu ambaye kama angeweza kumpa Mourinho miaka mitano kuna kila ushahidi kwamba si Barcelona , si Real Madrid wala Ac Milan au Manchester United ambao wangesimama mbele ya Chelsea kunako michuano ya ulaya . Makocha wote ambao wamepita Chelsea ukiacha Claudio Ranieri pekee ni washindi na ni watu ambao uwezo wao umedhihirika kwa wapenda soka wote , ni vipi waonekane vimeo Chelsea peke yake ?Jiulize kuwa kama usiku ule uliojaa mvua pale Moscow kwenye benchi la Chelsea kwenye uwanja wa Luzhniki angekuwepo Jose Mourinho na si Avrama Grant je matokeo yangekuwa kama yalivyokuwa kwa United kutawazwa mabingwa wa Ulaya, tazama rekodi ya Mourinho alipokuwa England dhidi ya Alex Fergusson na utapata jibu.
Andres Villas Boas anakuja Chelsea akiwa na heshima kubwa aliyojijengea mapema . Lakini atambue fika kuwa Abramovich ni kinyonga anayebadilika matokeo yanapokuwa mabaya na hatosita kushusha panga kwenye shingo ya kocha pasipo kumpa muda wa kuijenga timu , zaidi ya hapo ni mtu anayependa kuingilia majukumu ya kocha hasa linapokuja suala la usajili wa wachezaji . Kama kwa vikwazo vyote hivyo Andres Villas Boas atafanikiwa kumpa Roman ndoto yake ambayo ni ubingwa wa ulaya atakuwa ameandika ukurasa mpya si tu kwake binafsi kama kocha bali hata kwa makocha wa Chelsea chini ya mrusi Roman Abramovich .
Imeandaliwa na GEOFREY LEA
Mayb...!!! Time will TELL
ReplyDelete