Search This Blog

Wednesday, June 29, 2011

USAJILI WA BONGO UNAFUATA MAHITAJI AU SIASA MBELE.


Mara nyingi huwa napenda kuuzungumzia soka letu kwa kufananisha na sehemu zingine mathalani Ulaya , Afrika Kusini , Kenya na kwingineko, inaweza kuwa sio kitu sahihi lakini maendeleo endelevu hupimwa kwa kufananisha vitu viwili ili kuona kama viwango vya maendeleo husika vimefikiwa.

Kabla ya michuano ya Kagame Castle Cup soka lilikuwa limetawaliwa na taarifa za usajili . Timu mbalimbali zilikuwa kwenye harakati za kufanya usajili ili ‘kuimarisha vikosi vyao. Hapa kwenye usajili ndiyo hasa panaponitatiza . Kwa hali ya kawaida usajili hufanywa kwa kuzingatia mapungufu ambayo timu husika inayo . Mfano Manchester United kabla ya msimu kwisha walijua fika golikipa Edwin Van Der Saar angestaafu hivyo mapema walishafanya mipango ya kutafuta mbadala ,vivyo hivyo kwa Gary Neville ambaye hata kabla ya kustaafu kwake waliletwa vijana mapacha kina Da Silva ambao wamefanya vizuri na wameziba vizuri pengo la mkongwe Neville.
Mfano huu unakupa picha gani? Picha kubwa unayopata hapa ni kuwa klabu hii ina sera madhubuti ya usajili ambayo imesimamiwa na ndiyo kiini cha mafanikio ya muda mrefu ya timu hii na nyingine nyingi barani Ulaya .
Sasa kwa hapa nyumbani kwetu klabu huwa zinafanya usajili hovyo hovyo sana kiasi cha kumpa mtu maswali mengi ya kujiuliza . Watazame Simba msimu uliopita walimkosa mtu muhimu sana kwenye safu yao ya ulinzi , Mganda Joseph Owino , na kukosekana kwake kuliwaathiri sana na pengine ni moja ya sababu zilizopelekea kushindwa kuutetea ubingwa ilhali walikuwa na nafasi nzuri ya kufanya hivyo.


Haimaanishi kuwa Simba hakukuwa na mabeki , la hasha, ila mabeki wa aina ya Owino ndio waliokosekana . Walikuwepo Kevin Yondani , Meshack Abel na Juma Nyosso na hata Jerry Santo ambaye pamoja na kuwa kiungo ana uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kati . Mabeki wote waliotajwa hapo ni mabeki ambao wanacheza mtindo mmoja . Wote ni wakabaji wazuri na wana uwezo wa kumkalia mshambuliaji kooni . Ila wana upungufu mkubwa linapokuja suala la kuusoma mchezo na kujipanga wao kwa wao na ndio maana Simba haikupata matokeo mazuri katika mechi nyingi ambazo mabeki hawa walicheza pamoja.

Kwa kuona hili ungeweza kudhani kuwa Simba wangehitaji mtu kama Owino . Inawezekana ndio sababu iliyopelekea tetesi zakurejeshwa Victor Costa ambaye wote tunautambua uwezo wake . Lakini kurejeshwa kwa Costa kunamaanisha kuwa klabu hii itakuwa na mabeki sita wa kati kwani wapo kina Obadia Mungusa na Derick Waluhya walioongezwa . Sitamzungumzia Mungusa, tatizo langu liko kwa Derrick Waluhya . Huyu jamaa ni mgeni , raia wa Uganda ambaye uwepo wake unamaanisha kuwa Simba watalazimika kupunguza idadi ya wageni ambao walikuwa na mipango ya kuwasajili.

Sisemi kuwa Derick ni mchezaji mbaya , hapana , wala hiyo sio maana yangu ila nichojaribu kuonyesha hapa ni ukweli kuwa huu ni usajili usio na maana kwa Simba kwa kuwa sioni tofauti ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda na mabeki ambao tayari wako Simba . Kama ulitazama mchezo wa jumamosi dhidi ya Vital O ungeona ninaloongea .
Derick ni beki mwenye nguvu na anayeijua kazi yake ya kupambana kwani ni mpambanaji haswa ila mara zaidi ya moja yeye na Nyoso walikuwa wanaukimbiza mpira mmoja na mara zaidi ya moja alikuwa anajikuta analazimika kurudi nyuma kukimbiza washambuliaji wakati kama alikuwa anacheza na Nyoso alitakiwa kuwa nyuma yake ili asahihishe makosa yake kama Libero.
Waluhya alikuwa akishangiliwa sana na mashabiki kwani kazi yake ilionekana lakini naamini kwa asilimia zote kuwa kama ingalitokea Waluhya angecheza na mganda mwenzie Owino kwenye kikosi kimoja basi ukuta wa Simba usingepitika .

Uwepo Waluhya unamaanisha kuwa Simba haiwezi kusajili mshambuliaji tishio ambaye anaweza kuipa Simba mabao muhimu na kuponya ugonjwa sugu wa kina Mgosi wa kukosa magoli ugonjwa ambao umeigharimu mno Simba.
Hapo hapo Simba kuna kipa mpya toka Kenya anayeitwa Wilson Ochieng.kipa huyu amepewa kiasi cha doka elfu ishirini ($ 20,000) na mkataba wa miaka 3.


Ni kipa mzuri na rekodi yake inajieleza bila ubishi wala kificho kwani amewahi kucheza soka nje ya nchi yake na alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Kenya ambacho kilishiriki michuano ya kombe la mataifa ya afrika kwa mwaka 2004 nchini Tunisia. Lakini anakuja Simba ambako tayari yupo Juma Kaseja , kipa ambaye ni roho na uti wa mgongo wa timu , amechezea klabu hii kwa muda mrefu ana uwezo ambao haupishani sana na kipa huyu Mkenya.

Hivi Karibuni Kaseja ametia saini mkataba mpya wa miaka 2 kuitumikia Simba.Kaseja kwangu anabaki kuwa kipa bora na haingii akilini kumleta kipa mwingine tena kwa bei kubwa kama ilivyokuwa kwa Wilson Ochieng , jamani kipa wa akiba hawezi kuwa ‘high profile’ ,huwezi kukuta kipa namba moja kwenye timu ni Peter Cech halafu msaidizi wake ni David De Gea au Victor Valdez , hili linaweza kutokea tu kwenye timu ya taifa na si klabu ambapo unaweza kukuta kipa anacheza misimu mitatu bila kubadilishwa.Ni sera ipi iliyotumika kumsajili Wilson Ochieng?
Ndolo vs Niyonzima

Tuachane na Simba na tuhamie kwa mahasimu wao wakubwa Young Africans . Kuna majina matatu ambayo ni Kiza Hamis , Niyonzima Haruna na Ndolo . Kesi inayowahusu wachezaji hawa ni kwamba Yanga itakuwa na idadi ya wachezaji sita wa kigeni ilhali wachezaji wanaohitajika ni watano . Kati ya wachezaji hawa watatu kuna wawili ambao ni chaguo la kocha Sam Timbe na mmoja ambaye si chaguo la kocha ila ametokea kuteka hisia za viongozi,wanachama na mashabiki wa Yanga kiasi kwamba kama asingesajiliwa amani klabuni ingepotea . Hilo linakuonyesha kuwa hakuna sera ya usajili.Achana na kesi ya waganda hao wawili na Niyonzima , kuna jina ambalo halimo kwenye usajili wa Yanga msimu huu Ernest Boakye . Boakye kwa mtazamo wangu alikuwa mmoja ya wachezaji muhimu sana kwa Yanga na hata kwenye michezo dhidi ya Simba iliyochezwa msimu uliopita, Boakye alikuwa muhimu sana kwa Yanga kwenye nafasi ya kiungo, sijui kama kuna mchanganuo wa msimu uliopita na viongozi wa vilabu vyetu hivi juu ya michango ya wachezaji Fulani na umuhimu wao kwenye timu zao na ndio hasa ukafanyika usajili .
Usajili wa Humud Azam…

Ukiwatizama Azam msimu huu ni mojawapo ya timu ambazo zimefanya usajili makini sana , wanaye mshambuliaji hatari Kipre Tchetche ambaye naamini hataifaidi Azam kwa umahiri wake tu bali hata kiuchumi kwa sababu ana uwezo unaoweza kushawishi vilabu vikubwa nje ya nchi kumnunua japo Azam wana mafedha ya kutosha . Ila katika usajili huo kuna walakini kidogo . Mwaka jana Azam waliipiga bao Simba kwenye usajili wa Patrick Mafisango , mchezaji ambaye ni muhimu sana kwenye timu yoyote kutokana na uwezo wake wa kucheza mpira na kumudu nafasi nyingi uwanjani . Lakini msimu huu Azam wamembadili Mafisango na mchezaji toka Simba Abdulhalim Humoud . Humoud ni mchezaji mwenye kipaji halisi ambacho hakipingiki .Ila msimu uliopita haukuwa mzuri kwake akiwa Simba na kiukweli uwezo wake umeshuka kwa asilimia Fulani . Wenzetu ulaya huzingatia baadhi ya vitu kabla ya kumsajili mchezaji , vitu hivyo ni historia ya mchezaji , uwezo wake wa kucheza pasipo kuumia kwa muda mrefu na cha muhimu kabisa ni mchango wa mchezaji husika kwa timu anayotoka . Hii inamaanisha alicheza asilimia ngapi ya mechi za timu yake , kama alicheza mechi pungufu ya asilimia sabini na tano lazima uhoji mara mbili kabla ya kumsajili . Humoud alicheza mechi chache sana akiwa na Simba msimu uliopita na hilo linanipa maswali mengi kuhusu aliyefanya uamuzi wa kumsajili Azam. Ukiachana na mchango wa mchezaji kwa upande wa mechi kuna uwezo halisi wa mchezaji , Mafisango ana uwezo wa kumudu nafasi zaidi ya mbili uwanjani , humoud yeye anacheza nafasi moja tu ambayo ni kiungo wa kati , ina maana kuwa Simba wamepata faida ya kuwa na mchezaji ambaye ni sawa na wachezaji watatu ndani ya mchezaji mmoja .Kwa kutazama usajili ulivyofanyika ni dhahiri siasa zinatawala kuliko ufundi , je soka letu litapiga hatua kwa mtindo huu?

1 comment:

  1. Kwa upeo wangu ni siasa tu ili either uongozi fulani uwepo madarakani au kiongozi individual,that's why tunabahatisha tu hasa kwenye yanga na simba.
    Nasema sababu,Sijawahi kusikia kuna mtaalamu wa soka kaenda nchi fulani akitokea kwenye hivi vilabu ili kumtathmini mchezaji fulani akicheza kwenye ligi fulani kwa mechi kadhaa.
    Zaidi ya kusikia viongozi ndio anaenda leo na kesho kaona mchezaji anasajiliwa,natoa mfano;kuna mchezaji u21 wa Denmark wanachama wa man utd wamemwona wanamchambua kupitia mtandao wa timu yao kumshawishi kocha amsajili,wanamwambia kocha "vitu vilivyopungua kwa huyo dogo vinajengeka kwa mafunzo coz umri wake unaruhusu,fergie katuma mtu achunguzwe.
    Sisi tutaendelea kuwapata wakina Mba wengi tu kwa style hii,Nimesikia kocha wa simba kasema asajili mtu mpaka amjaribu,that's very right kama akilimudu hilo.
    Nakubali azam wako makini coz Ukiingia kwenye mtandao wao wamenyamnua kila mchezaji why kasajiliwa na Leo hii wao hawapo kwenye kagame CASTLE cup lakini wameshaanza program ya ligi,simba na yanga hazijui hata majina ya kuwasilisha TTF!!!!!
    Ila dirisha bado liko wazi waendelee kubahatisha.....
    Big up Azam,naona mabadiliko ya soka mbeleni via Azam

    ReplyDelete