Aliyekuwa mchezaji wa kutumainiwa wa Klabu ya APR ya Rwanda HARUNA NIYONZIMA amewasili rasmi nchini akitokea nchini humo ili kujiunga na Young Sports Club ya Mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Shaffih Dauda Blogspot, NIYONZIMA amesema amewasili nchini ili kuitumikia klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuiwezesha kupata mataji mbalimbali ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mchezaji huyo aliyepokelewa na viongozi mbalimbali wa Klabu ya Yanga, alikuwa akitajwa mara kwa mara na mashabiki wa timu hiyo kwamba atajiunga na vijana wa jangwani ili kukiongezea nguvu kikosi hicho.
“Nimekuja nchini kufanya kazi na si vinginevyo, soka linachezwa popote ninachoomba ni ushirikiano kutoka kwa mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu kwani bila ushirikiano siwezi kufanya lolote Jangwani,” alisema NIYONZIMA.
Akifafanua mchezaji huyo wa kimataifa amesema, yeye sio Mungu na anayeweza kufanya maajabu akiwa klabuni hapo.
Kutokana na hilo alisisitiza kutumia uwezo wake kwa ushirikiano na wachezaji wenzake ili kupata mafanikio.
Kuhusiana na Michuano ya Kombe la Kagame Castle Cup inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni katika viwanja mbalimbali ikiwemo Taifa na Jamuhuri mkoani Morogoro, NIYONZIMA amesema hilo liko chini ya viongozi wa klabu ya Yanga.
“Siwezi kusema kama nitashiriki kwenye michuano ya Kombe la Kagame, mimi ni mwajiriwa wa Jangwani kwa sasa hivyo wao ndio watakaoamua nani wa kucheza au lah,” alibainisha mchezaji huyo.
Wakati huo huo alizungumzia mustakabali wake wa baadae kuhusiana na soka na kusema anaiheshimu kazi hiyo kwa kuwa ndio inayompa fedha za kujikimu kimaisha ikiwemo kuhudumia familia yake.
Hivyo amejiunga na Yanga baada ya kupata ushauri kwa marafiki zake ikiwemo wachezaji wenzake wanaocheza soka nchini ambao wamempa moyo kwamba atafanya vizuri akiwa na timu hiyo.
Kuhusiana na kama atarudi APR ya Rwanda mara baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika NIYONZIMA amesema hatarajii kufanya hivyo kwani kitendo cha kuondoka hakikuwafurahisha viongozi wa timu hiyo.
“Ni vigumu kuzungumzia hali ya baadae kimpira, ila kwa kuwa ni mchezo lolote linaweza kutokea. Nimeondoka APR huku viongozi wangu wakiwa na kinyongo,” alimalizia.
No comments:
Post a Comment