Moses Basena-Kocha wa Simba
Kuelekea kwenye mchezo wa marudiano wa michuano ya kombe la shirikisho ambapo wawakilishi pekee waliosalia wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Simba Sports Club watakuwa wanavaana na timu ya Dc Motema Pembe toka Congo ( Jamhuri ya Kidemokrasia) Blog yako maalum kwa masuala ya michezo imeandaa uchambuzi mfupi wa baadhi ya mambo ambayo Simba wanapaswa kuzingatia ili kuingia kwenye hatua ya makundi ya kombe la shirikisho .
1.Simba wanapaswa kuelewa kuwa huu ni mchezo wa ugenini.
DC Motema Pembe ina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka pengine hata kuliko wachezaji wengi wa Simba na ninaposema wana uwezo pengine kuwazidi wachezaji wa Simba simaanishi kuwa Simba haina wachezaji wenye uwezo ila kwa mchezo uliochezwa Jumapili iliyopita Dc Motema Pembe walicheza kwa mbinu na ufundi wa hali ya juu mno.
Kila mchezaji anatambua jukumu lake na analitekeleza kwa ufanisi wa asilimia mia moja hamsini. Kama Simba wakitambua kuwa wanacheza na timu yenye uwezo mkubwa wanapaswa kufanya kila liwezekanalo kucheza kama inavyopasa kucheza ukiwa ugenini . Ukirejea nyuma kwenye msimu wa mwaka 2007/2008 ambapo Manchester United walitwaa ubingwa wa ulaya walikutana na Inter Milan kwenye hatua ya Robo Fainali.
Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa kule Milan Sir Alex Fergusson alipanga kikosi ambacho mtazamo wake ulikuwa ulinzi kwanza , kwa jinsi United ilivyokuwa kwenye fomu kipindi kile wangeweza kushinda mchezo ule lakini haikuwa kwenye mipango ya Fergie kujilipua na kushambulia mwanzo mwisho , alichezesha timu ambayo ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa wavu hauguswi na hilo lilitimia.
Hivyo Simba wanapaswa kwenda wakiwa na jukumu la msingi ambalo ni kuhakikisha Juma Kaseja haokoti mpira ukiwa umeingia wavuni bali analindwa kiufundi .Kwa msimu huu pekee Simba imecheza mechi zisizopungua tatu za kimataifa nje ya mipaka ya Tanzania na ningependa kuamini kuwa wachezaji wa Simba wamejifunza kitu kwenye mechi hizo hivyo ni vyema wakacheza kama inavyopaswa kucheza unapokuwa ugenini .
2. Akili ya ziada ya kucheza soka tofauti na lile walilozoea kwa kawaida.
Simba ni klabu ambayo ina falsafa ya kucheza soka la kuvutia , kushambulia kwa uvumilivu huku wakitumia viungo wenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuuchezea kama watakavyo , lakini kwa mchezo wa ugenini hii haitakuwa jambo la busara sana kwani Dc wana uwezo wa kufanya lolote na kitibua sherehe ambayo Simba wako njiani kuiandaa.
Kwenye mchezo wa Jumapili Simba hawana budi kucheza kwa tahadhari ya hali ya juu sana wakitambua fika kuwa wanatafuta aina Fulani ya matokeo . Mara nyingi mbinu kuu ya ulinzi kwenye soka ni mashambulizi lakini Simba sasa haina Mbwana Samatta mmoja wa wachezaji wachache wenye uwezo wa kufunga pale anapotaka kufanya hivyo ,hivyo kutokana na hazina ya bao moja ambayo ipo ni vyema falsafa ya Simba ikabadilika japo kwa dakika tisini tu.
3. kuchezesha viungo watano.
Ukitazama safu ya kiungo ya Simba kwenye mchezo wa kwanza ilionekana kupwaya sana . Mohamed Banka na Nico Nyagawa walionekana kuelemewa mwishoni mwa mchezo.Sababu kuu ya hili ni ama kukosekana kwa Jerry Santo au umri wao mkubwa unaweza kuwa uliwagalimu viungo hawa.
Santo anacheza kama kiungo wa kukaba alikosa mchezo huo kutokana na kuwa na kadi mbili za manjano. Ni vyema kocha akatambua mchango wa Santo kwa Simba na kumpa nafasi yake kwenye kikosi kitakachocheza.
Lakini pia ili kuwanyima mwanya viungo DCMP wakiongozwa na (NDANDA KOSOVO na KANU) ambao walitumia vyema maumbo yao dhidi ya maumbo madogo ya kina Banka na Nyagawa,
Ili simba iweze kuwadhibiti inatakiwa kuwa na viungo watano Amir Maftah acheze kiungo cha kushoto,Shija Mkina kiungo cha kulia,katikati wacheze santo,nyoso na mbele yao acheze Amri Kiemba.
Santo ana umbo kubwa kama la KANU wa Motema Pembe hivyo kama akipewa jukumu la kucheza naye bluzi (kumkaba ng’ado kwa ng’ado yaani ‘zero distance ‘ kama wafanyavyo maharusi wakicheza blues) tatizo kubwa lililoikabili Simba kwenye mchezo wa kwanza litakuwa limesuluhishwa.
4. Kuepuka kutoa mipira na kucheza madhambi karibu na eneo la hatari.
Unaweza ukashangazwa na hili lakini linaweza kuidhuru Simba . Dc motema Pembe wana mtu ambaye anarusha mipira kwa staili ya aina yake .Jamaa anabinuka sarakasi anaporusha na mipira yake inaenda kwa spidi ya hatari kutokana na nguvu za ziada anazozitumia zinazoupa mpira spidi ya ajabu .
Mipira anayorusha huyu jamaa inaenda kama kona vile na kama ikitokea Simba wakawa wanatoa mipira karibu na eneo la hatari wanaweza kujikuta wakiwapa wapinzani faida kwa kuwa mipira inayoweza kusababisha kizaa zaa kwenye lango la Simba,Pia simba wanatakiwa kuwa makini sana na kufanya madhambi karibu na goli lao.
5. Ally Shiboli aanze badala ya Emanuel Okwi.
Hakuna uficho kuwa Emanuel Okwi alikuwa nyota wa mchezo wakati timu hizi mbili zilipokutana wiki iliyopita . Alikuwa akiifanya ngome ya Motema Pembe kama alivyokuwa anataka na kama Simba wangekuwa makini wangeondoka na ushindi mnono zaidi siku ile kutokana na nafasi nyingi alizokuwa anatengeneza okwi.pia Okwi alicheza vizuri dhidi ya TP Mazembe mchezo uliofanyika huko Lubumbashi,
Kwa hakika Motema Pembe lazima watakuwa wamemtazama kwa karibu mganda huyu na kumtengenezea mbinu za kumkabili wakijua kuwa ndiye anayeweza kuwa tishio hiyo Jumapili.
Kama ningekuwa kocha wa Simba ningecheza na akili zao kisaikolojia kama anavyofanya Jose Mourinho au Sir Alex Fergusson. Kwa vyovyote Simba watafanya mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo hivyo nigeenda na okwi na kumpa nafasi ya kuwa mzungumzaji mkuu na ningemwambia awaeleze waandishi kuwa ataongoza mashambulizi siku ya mchezo . Kwa vyovyote Motema Pembe wataingia na akili ya kumkabili kwa kuwa watatumia muda mwingi kutazama jinsi ya kumkabili lakini siku ya mechi anaanzia benchi na nafasi yake nampa Shiboli ambaye ana kasi na nguvu.
Kwa kifupi Simba wanatakiwa kujua kuwa wanaingia kutupa karata ya mwisho na karata hii ndio yenye uhai wao linapokuja suala la michuano ya kimataifa , michuano ambayo kwa msimu huu ulioisha imewapa Simba faida ya kujipatia fedha nyingi kutokana na mauzo ya Mbwana Samata na Patrick Ochan waliouzwa baada ya kung’aa kwenye mchezo dhidi ya Tp Mazembe . Huwezi jua pengine kuna vilabu vingine vinavyoweza kuwaona kina Kaseja,okwi,Santo ,Amir Maftah na wengine wakiichezea Simba kwenye hatua ya makundi ya kombe la shirikisho , lakini nafasi hii itakuja kutokana na jinsi watakavyocheza siku ya jumapili ,
6.Seleman Matola kuwepo kwenye benchi la ufundi.
Kwenye mchezo wa kwanza moja kati ya matatizo niliyoyaona ni kukosekana mzawa kwenye benchi la ufundi la Simba ambaye anatakiwa kuwa anawasiliana na wachezaji mara kwa mara wakati mchezo ukiendelea.
Kwa mtizamo wangu Seleman Matola ndiye anayefaa kwenye jukumu hilo,akiwa kama nahodha mwenye mafanikio kuliko wote kwenye historia ya Simba,kitu ambacho kinamfanya kuwa na heshima kikosini.
Mungu Ibariki Simba, Mungu Ibariki Tanzania .
Kweli kaka Simba wanahitaji kuchezesha viungo watano kuwashield mabeki coz pamoja na yote beki za kati za simba ni tetenasi,But mimi hua namkubali sana Abdulahim Humud mbona hachezeshwi au ndo tuseme ameshindwa kuperfom kiivyo au majungu,Kwangu mimi namuona anafaa sana kwenye kiungo cha kukaba na angechezeshwa badala ya nico Nyagawa coz siku hizi Nyagawa hana pumzi ananoki ndani ya dakika 20 za mwanzo
ReplyDeleteWachezaji wetu bado sana Tanzania na hii inaonesha wanshindwa kutumia akili zao kucheza mpira, nikisema hivi maana yake ni kwamba wenzao kama ulivyosema kila mtu alitimiza jukumu lake, hivyo wachezaji wetu hawa hawawezi kutimiza jukumu mara nyingi wanajisahau na wanashindwa kuona jukumu la kucheza ugenini kuzuia zaidi na kushambulia kwa kushtukiza, hata hivyo imani yangu ni kwamba Simba tayari imeshatolewa na DC Motema Pembe, endapo Patric Phir angekuwepo pengine timu hii ingeitoa Wadad Casablancsa, asante
ReplyDelete