Search This Blog

Friday, June 24, 2011

KAGAME CASTLE CUP PREVIEW

MABINGWA mara sita wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Simba SC ‘Wekundu wa Msimbazi’, Jumamosi hii wanafungua dimba la michuano hiyo inayojulikana Kombe la Kagame tangu mwaka 2002, kwa kumenyana na Vital’O ya Burundi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba walio chini ya kocha Mganda, Moses Bassena watamenyana na Vital’O timu ambayo pamoja na kuwa na historia ya kucheza soka tamu kwenye michuano hii, lakini hawajawahi kutwaa taji, siku moja kabla ya watani wa wa jadi, Yanga kucheza mechi yao ya kwanza na el Merreikh ya Sudan.
Hadi leo bado haikuwa imejulikana ni wachezaji gani (20) ambao Simba imetuma majina yake CECAFA kwa ajili ya kuwatumia kwenye michuano hiyo, lakini katika wachezaji wapya, shaka ipo kwa beki Shomari Kapombe wa Polisi Moro na kiungo Mwinyi Kazimoto tu iliyemsajili kutoka JKT Ruvu, kutokana timu za za jeshi kuweka ngumu, kwa kudai ni waajiriwa wa taasisi hizo na hawawezin kufanya kazi uraiani.
Wachezaji wengine wapya wa Simba, kipa Mkenya, Willies Ochieng, aliyekuwa anacheza soka ya kulipwa Finland, mabeki Obadia Mungusa ‘Robot’ wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Nassor Masoud ‘Choro’ wa JKT Oljoro, viungo Haruna Moshi ‘Boban’ mchezaji huru, Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga na Salum Machaku wa JKT Ruvu.
Bassena ataunganisha wachezaji hao na wale aliowakuta kwenye klabu hiyo akina Juma Kaseja, Salum Kanoni, Amir Maftah, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Jerry Santo, Mohamed Banka, Amri Kiemba, Emmanuel Okwi, Mussa Mgosi, Shija Mkina, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Nico Nyagawa kupata nyota wa kucheza Kombe la Kagame.
Kwa vyovyote, mechi ya Jumamosi inatarajiwa ngumu kwa Simba, kwani Vital’O ambayo imecheza Robo Fainali tatu za michuano ya klabu Afrika, Ligi ya Mabingwa mwaka 1985 na lililokuwa Kombe la Washindi mara mbili katika miaka ya 1983 na 1990 miaka yote imekuwa ikitoa ushindani na kuonyesha soka safi, ingawa kutwaa taji ndio imekuwa mtihani mgumu kwao
.

Vital'O FC iliyoanzishwa kama Rwanda Sport FC miaka 1960, kabla ya kuwa ALTECO mwaka 1971, baadaye Tout Puissant Bata mwaka 1973, kisha Espoir kabla ya kuanza kutumia jina lake la sasa (Vital'O) mwaka 1975, itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa na Simba 1-0 zilipokutana mara ya mwisho kwenye michuano hii, Julai 20, mwaka 2008 Dar es Salaam, bao pekee la beki Kelvin Yondan dakika ya 42, mchezo wa Kundi A, ulioihakikishia Simba tiketi ya kuingia Robo Fainali.
Simba, ambao ni mabingwa mara nyingi wa michuano hii, pia ndio timu ya mwisho ya Tanzania kuchukua Kombe la Kagame wa 2002 visiwani Zanzibar, ikiiwafunga 1-0 Prince Louis ya Burundi, bao pekee la Nteze John dakika ya sita, kikiosi cha Wekundu wa Msimbazi kikiundwa na Mohamed Mwameja, Said Sued, Ramadhan Ramadhan aliyetoka na kumpisha Majuto Komu dakika ya 35, Amri Said, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Stephen Mapunda ‘Garrincha’ aliyempisha Joseph Kaniki ‘Golota’ dakika ya 74, Shekhan Rashid, Yusuf Macho, Nteze John aliyempisha Emmanuel Gabriel dakika ya 61 na Mkenya Mark Sirengo
YANGA V EL MERREIKH:
Yanga, wanaorejea kwenye michuano hiyo tangu washiriki kwa mara ya mwisho mwaka 2008 na kukomea Nusu Fainali, watafungua dimba na El Merreikh ya Sudan kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, siku ambayo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro watetezi wa taji, APR watamenyana na Ports.
Unatarajiwa kuwa mchezo mwingine mkali na wa kihistoria, kwani utawakumbusha mashabiki wa Yanga fainali ya michuano hiyo, mwaka 1986 Abubakar Salum ‘Sure Boy’ akiwa bado mbichi anaingia kutokea kwenye benchi na kufanya mambo makubwa, lakini mwishowe yeye mwenyewe anaharibu.
Sure Boy alitokea benchi Yanga ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 na kusawazisha yote, lakini mchezo ulipohamia kwenye mikwaju ya penalti winga huyo matata wa zamani pamoja na kiungo Muhiddin Cheupe walikosa penalti zao, Yanga ikilala 4-2 na kukosa Kombe nyumbani.
Lakini ubabe wa Merreikh kwa Yanga uliendelea tena mwaka 2007 katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika walipowatoa mabingwa hao wa Bara kwa jumla ya mabao 2-0, wakianza na sare ya bila kufungana Uwanja wa Kirumba mwanza, mechi ambayo aliyekuwa mfadhili wa Yanga, Yussuf Manji aliinunua kwa Sh. Milioni 100 na mashabiki wakaingia bure.
Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ wakati huo, ilitoka kutolewa na Esperance ya Tunisia katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa kwa kichapo cha mabao 3-0.
Yanga ipo Kundi B na El Merreikh ya Sudan, Bunamwaya ya Uganda na Elman ya Somalia, wakati Simba SC ipo Kundi A na Vital’O ya Burundi, Etincelles ya Rwanda na Ocean View ya Zanzibar na mabingwa watetezi, APR wamepangwa kundi C pamoja na St George ya Ethiopia, Ulinzi ya Kenya na Ports ya Djibouti.
Timu mbili za juu katika kila kundi, zitafuzu moja kwa moja kuingia Robo Fainali, wakati washindi wa tatu wa makundi yote watalinganishwa kwa wastani wa pointi ili kupata timu nyingine mbili za kutinga Robo Fainali, zitakazochezwa Julai 4 na 5 na kuonyeshwa moja kwa moja (live) na Televisheni ya Supersport ya Afrika Kusini.
Nusu Fainali zitachezwa Julai 6 na 7 na mechi ya kusaka mshindi wa tatu pamoja na fainali zitachezwa Julai 9, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Michuano ya Kagame ilianza kama Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, mwaka 1974 kabla ya kuwa Kombe la Kagame mwaka 2002, kufuatia Rais wa Rwanda, Paul Kagame kuamua kudhamini michuano hiyo.
Simba inaongoza kuchukua taji hilo mara nyingi, mara sita, ikifuatiwa na AFC Leopards mara tano sawa na Tusker FC zote za Kenya, Yanga mara tatu sawa na APR FC, Gor Mahia ya Kenya na SC Villa ya Uganda, wakati Luo Union na El-Merreikh zimetwaa taji hilo mara mbili na ATRACO ya Rwanda, KCC, Police FC za Uganda na Rayon Sports zimetwaa mara moja kila moja.
Timu ya mwisho ya Tanzania kutwaa taji hilo ni Simba SC mwaka 2002 visiwani Zanzibar, wakati miaka miwili mfululizo iliyopita taji liliweka maskani Rwanda, 2009 kwa ATRACO na 2010 kwa APR.

No comments:

Post a Comment