Search This Blog

Wednesday, June 15, 2011


Kwanini vilabu vikubwa ulaya vinauana kumpata?
Alexis Sanchez ni mchezaji mwenye umri wa miaka 22 . Sanchez ni raia wa Chile na anacheza kwenye klabu ya Serie A Udinese. Ulimwengu ulimshuhudia Sanchez kwa mara ya kwanza akipeperusha bendera ya taifa lake la Chile kwenye Kombe la dunia mwaka jana ambako Chile ilifika hatua ya 16 bora.

Tangu hapo Sanchez amepiga hatua mara dufu , msimu huu ulioisha Sanchez alifunga mabao 12 kwenye michezo 31 ikiwemo mechi moja dhidi ya Palermo ambapo alitupia bao nne na hatimaye kuisaidia Udinese kufuzu kucheza ligi ya mabingwa barani ulaya .

Mabingwa wa England mashetani wekundu Manchester United na jirani zao Manchester City hivi sasa wapo kwenye ushindani mkubwa sana wa kuipata saini ya Alexis Sanchez huku Barcelona , Real Madrid na Inter Milan wote wakimtazama kwa karibu japo United wanaonekana kuongoza mbio za kumsajili baada ya Sanchez mwenyewe na wengi wa washauri wake na watu wa karibu kumshauri aende kwa ‘babu fergie’.
Sanchez kwa asili ni winga lakini ana uwezo wa kucheza katikati nyuma ya mshambuliaji na anatumia miguu yote .

Uwezo gani hasa?
Watu wengi wamekuwa wakisema kuhusu uwezo wa Sanchez na karibu msimu mzima wa Serie A ulioisha hivi karibuni kivutio kikubwa kilikuwa uwezo wake wa kuwapita mabeki na kumiliki mpira bila wasiwasi na hakika Sir Alex Fergusson ameyasikia yaliyosemwa .
Sanchez alianza kucheza soka kama winga wa kulia lakini kadri alivyoendelea kupata uzoefu amekuwa akitumika kwenye maeneo mengi kwenye upande wa juu wa uwanja.

Alexis sio mshambuliaji kabisa ni aina ya watu ambao nchini uholanzi wanaitwa “mshambuliaji wa uongo” (yaani mtu anayetumika kama mbadala wa mshambuliaji –mara nyingi kiungo mwenye uwezo wa kufunga) ila anaweza kucheza kati nyuma ya mshambuliaji mkuu na kwa United mfano wa anavyocheza Wayne Rooney United .
Sanchez anaonekana kama Cristiano ronaldo mwingine. Hii ni kwa jinsi anavyopenda vibaiskeli na pia analijua goli lilipo na uwezo wake wa kufunga unajulikana kama unabisha waulize Palermo
.



Sanchez Ni Ronaldo mwingine?
Wengi wamemtazama Alexis Sanchez kama Cristiano Ronaldo mwingine na kama ukichukua muda wako kutazama clip ambazo tumeziweka hapa kwenye blog utaona kwanini .
Ana mtindo flani wa kuchezea mpira kama wa CR7 japo kwenye ligi ya Italia wengi walimfananisha na Lionel Messi kwa jinsi alivyo na miguu yenye kasi lakini Sanchez mwenyewe hapendi kufanishwa na wachezaji hao wawili ila kama ataiteka ligi kuu ya England kama alivyofanya Ronaldo Manchester patakuwa mahala sahihi .

Je amekamilika kuikabili ligi ya England?
Vilabu viwili vya Manchester pengine vinatambua kwa uthibitisho na ushahidi wa kutosha juu ya hatari zinazowakabili wachezaji wenye asili ya amerika ya kusini pindi wanapokuja England.
Nyota wa Uruguay Diego Forlan alishindwa kuwika United wakati Carlos Tevez ameweza kun’gaa akiwa United na City.


Robinho aliyekuja Man City kwa thamani ya paundi million 32.5 alikuwa tatizo huko Eastlands .
Sanchez mwenyewe angependelea kubakia Italia au kwenda Barcelona ila Manchester United wanaweza kumfanya abadili mawazo yake .

Kwa umbo lake la futi 5 na nchi 6 ni dhahiri mabeki wa England kina Gary Cahill na Christopher Samba watampa wakati mgumu kwa mabuti yao ya hatari ila watalikoga vumbi la kutosha kutokana spidi aliyo nayo , pamoja na umbo dogo alilonalo Sanchez ana nguvu na ufupi wake mara nyingi unamuongezea stamina na balance ya kuhimili rafu .

Ataenda wapi mwisho wa siku?
Alama za nyakati zinaashiria kuwa Man United watawazidi mahasimu wao Man City kete kwa kumnasa Sanchez kwa sababu kwa kitita cha fedha ambacho kimiwekwa kwa ajili ya Barcelona kufanya usajili ni dhahiri hakitatosha kumnasa na hata Barca wakikomaa na kumsajili Sanchez ataenda kucheza wapi zaidi ya kukalia benchi jambo ambalo hata yeye mwenyewe asingependa kulipitia , Madrid wana mipango mingine na hawajajihusisha kabisa na Sanchez , Manchester City wameweka ubaoni kitita cha paundi million 30 na wanaweza kuongeza wakihitajika kufanya hivyo lakini ushawishi mkubwa wa Manchester United kupitia mafanikio waliyo nayo nambinu ujanja wa Sir Alex Fergusson na mkurugenzi wake bwana David Gill ni dhahiri vitatosha kumleta Sanchez Old Trafford

No comments:

Post a Comment