inahofiwa idadi ya waliokufa huenda ikaongezeka.
Watu 74 wamefariki kufuatia ghasia kati ya mashabiki wa timu mbili katika mji wa Port Said, nchini Misri.
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa televisheni ya taifa.
Watu hao walikiufa baada ya mashabiki kuanza kuingia uwanjani, baada ya mechi kati ya vilabu viwili vikuu vinavyoongoza ligi nchini humo, Masry na Al-Ahly, siku ya Jumatano.
Inahofiwa kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka, kwani zaidi ya watu 156 wamejeruhiwa.
Huu ndio msiba mkubwa zaidi nchini Misri kuwahi kutokea katika uwanja wa kandanda, alielezea naibu waziri wa afya nchini Misri.
“Huu ni msiba wa kusikitisha mno”, alisema Hesham Sheiha kupitia matangazo ya televisheni.
Kati ya waliokufa ni pamoja na maafisa wa usalama.
Mwandishi wa BBC anaelezea kwamba ukosefu wa usalama mkali ambao hudumishwa kwa kawaida huenda ikawa ni jambo ambalo lilichangia kutokea ghasia hizo.
Polisi nchini Misri wametulia mno tangu kufanyika maandamano yaliyomtoa Rais Hosni Mubarak madarakani.
Katika mechi hiyo ya Jumatano, timu ya Port Said, Masry, ilipata ushindi wa magoli 3-1.
Walioshuhudia walielezea kwamba kulikuwa na hali ya wasiwasi muda wote wa mechi hiyo, tangu shabiki mmoja wa Al-Ahly alipoinua bango ambalo inadaiwa lilikuwa linawatukana mashabiki wa timu ya nyumbani.
Katika mitandao ya jamii, licha ya kutokuwepo ushahidi, uvumi umekuwa ukienea kwamba maafisa wa usalama walikuwa wanapanga njama ya kupambana na mashabiki wa Al-Ahly.
Maafisa wachache wa polisi walijitahidi kuwapa ulinzi wachezaji, lakini hawakufanikiwa kabisa.
Sehemu moja ya uwanja ilichomwa moto.
Maafisa wanaohusika wameelezea kwamba vifo vingi vilitokana na watu kupata majeraha makubwa ya kichwa kwa kupigwa au kukatwa, na wengine kuzimia hadi kufa wakati wa mkanyagano.
Ndege za helikopta zilitumwa hadi Port Said kuwasafirisha hadi hospitali mashabiki waliojeruhiwa.
"Huu si mpira. Hivi ni vita na watu wanakufa mbele yetu", alisema mchezaji wa Al-Ahly, Mohamed Abo Treika.
Mbunge wa Port Said, Albadry Farghali, aliwalaumu maafisa wa usalama.
"Walikuwa wapi haya yote yakitokea?"
"Watu wa Mubarak bado wako uongozini. Kiongozi wa utawala ameng'atuliwa, lakini watu wake bado wapo madarakani", alielezea kupitia televisheni.
"Usalama uko wapi? Serikali iko wapi?"
Mjini Cairo, mwamuzi alisitisha mechi nyingine, alipoarifiwa juu ya ghasia za Port Said.
Jambo ambalo liliwafanya mashabiki kuchoma moto sehemu fulani za uwanja.
Mechi zote za ligi kuu zimefutiliwa mbali, na bunge jipya la Misri siku ya Alhamisi litakutana katika kikao cha dharura kuujadili msiba huu.
Source: bbcswahili.com
No comments:
Post a Comment