ZIKIWA zimesalia siku nne kabla ya kumenyana na timu ya soka ya Taifa,
Taifa Stars, Kocha wa Ivory Coast Francois Zahoui ametimuliwa kazi.
Stars inatarajiwa kusafiri keshokutwa kuelekea Abidjani kwa ajili ya
kumenyana na Ivory Coast katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya
Kombe Dunia itakayochezwa Juni 2.
Habari kutoka Ivory Coast zilisema jana Shirikisho la Soka la nchi
hiyo (FIF) limemfuta kazi kocha huyo saa 24 baada ya timu yake kunyukwa
mabao 2-1 na Mali katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Ufaransa.
Mchezaji wa zamani wa Ufaransa Sabri Lamouchi ndio ametangazwa kuwa
kocha mpya wa Tembo hao ambaye ataiongoza timu hiyo katika mechi za
kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 pamoja na ile ya Kombe la
Mataifa Afrika 2013.
Uteuzi wa kocha huyo mwenye umri wa miaka 40 ambaye amewahi kuwa
kiungo wa Auxerre, Monaco, Inter na Marseille umeshtua wengi kwasababu
hakuwa kwenye orodha ya waliokuwa wakitarajiwa kuchukua nafasi hiyo kama
ilivyokuwa kwa kocha wa zamani wa Senegal Bruno Metsu, Eli Baup,
Antoine Kombouaré na kocha wa zamani wa England Sven Goran Eriksson.
Lamouchi alistaafu kucheza soka ya kimataifa mwaka 2001 baada ya
kucheza mechi 12 tu dhidi ya Les Bleues na kufunga bao moja, hajawahi
kuifundisha timu yoyote ya taifa.


No comments:
Post a Comment